Serikali : Hakuna mtoto kukosa darasa

KUELEKEA kufunguliwa kwa muhula mpya wa masomo Januari 13, 2026, taswira ya elimu nchini inaonesha mafanikio makubwa yanayopaswa kupongezwa na kulindwa kwa vitendo. Serikali, kupitia jitihada za uongozi wake kuanzia ngazi ya kitaifa hadi mikoa na wilaya, imefanikiwa kutatua moja ya changamoto sugu katika sekta ya elimu ambayo ni uhaba wa madarasa.

Sasa, watoto wanaelekea shuleni wakiwa na uhakika wa miundombinu iliyokamilika kwa wakati na inayotosha mahitaji halisi. Mfano hai ni Mkoa wa Dar es Salaam ambako wanafunzi 95,323 wanatarajiwa kuanza kidato cha kwanza, huku zaidi ya wanafunzi 132,000 wakijiandaa kuanza darasa la kwanza.

Kinyume na hofu za awali, mkoa huo sasa una madarasa 1,941 dhidi ya mahitaji ya 1,907, ikiwa ni ziada ya madarasa 34. Huu ni ushahidi wa mipango madhubuti, utekelezaji wa haraka na dhamira ya dhati ya serikali kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa nafasi ya kujifunza kwa kisingizio cha miundombinu. Hatua ya serikali kuondoa kabisa utaratibu wa kuwachangisha wazazi michango ya ujenzi wa madarasa katika mazingira ambayo madarasa tayari yapo ni ya kuigwa.

Inalinda haki ya mtoto kupata elimu bila vikwazo visivyo vya lazima na inaleta uwazi katika usimamizi wa shule. Ni wajibu wa wakuu wa shule kuzingatia msimamo huu na kushirikiana na wazazi kwa uadilifu pale tu inapohitajika makubaliano halali. Mafanikio haya hayaishii Dar es Salaam pekee. Mikoa mingine, ikiwemo Ruvuma, Mbeya na Dodoma, imejipanga kuhakikisha muhula unaanza kwa wakati na kwa ufanisi. SOMA: Manispaa Geita yawahakikishia usalama wahitaji shuleni

Kauli za viongozi wa mikoa na wilaya zinabeba ujumbe mmoja ulio wazi, miundombinu ipo, walimu wapo, sasa ni zamu ya wazazi na walezi kutimiza wajibu wao. Mtoto ana haki ya msingi ya elimu, na haki hiyo haiwezi kuachwa ikitegemea uzembe au visingizio vya mtu mzima. Ni jambo la msingi kusisitiza kuwa hatua za kisheria dhidi ya wazazi au walezi wanaoshindwa kuwapeleka watoto shuleni si adhabu bali ni ulinzi wa mustakabali wa taifa.

Elimu ndiyo mtaji mkuu wa maendeleo, na taifa linaloruhusu watoto wake kubaki nje ya mfumo wa elimu linajiwekea mzigo wa umaskini, ujinga na ukosefu wa ujuzi katika siku zijazo. Kwa upande mwingine, walimu na watendaji wa shule wana wajibu wa kitaaluma na kimaadili kuhakikisha hakuna mtoto anayerejeshwa nyumbani kwa sababu yeyote ile isiyo halali.

Mtoto anayefika shuleni anapaswa kupokelewa, kusikilizwa na kusaidiwa, si kukatishwa tamaa. Maelekezo ya wazi yametolewa, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtumishi au mwalimu atakayemrudisha mtoto nyumbani bila sababu za msingi. Nidhamu hii inalenga kulinda maslahi ya mtoto na kuimarisha uwajibikaji katika mfumo mzima wa elimu. Kwa ujumla, kukamilika kwa ujenzi wa madarasa kwa wakati ni ushindi mkubwa wa sera, bajeti na usimamizi.

Ushindi huu utakuwa na maana halisi pale tu wazazi watakapowapeleka watoto shuleni, walimu wakawapokea kwa moyo wa huduma, na viongozi wakasimamia utekelezaji bila kuyumba. Januari 13, 2026 si tarehe ya kawaida, ni mwanzo wa safari mpya kwa maelfu ya watoto na ni kipimo cha namna taifa linavyothamini elimu kama msingi wa maendeleo yake ya sasa na ya baadaye.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button