Wazazi watakiwa kusimamia watoto Mikindani

BAADHI ya wazazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha watoto waliyositisha masomo kwenye shule za sekondari wilayani humo kutokana na changamoto mbalimbali warudi tena shuleni ili wakaendelee na masomo yao.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wazazi hao yaliyofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kuhusu kuwajengea uelewa zaidi wazazi hao waone umuhimu wa elimu, Mratibu wa Mradi wa ‘Rudisha Msichana Shule’ Theresia Mpinga amesema wazazi hao wahamasike na kuhakikisha watoto wao wanarejea shule wakapate elimu ili waweze kufikia ndoto zao.
Mafunzo hayo yametolewa na Shirikia lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala mbalimbali ya kijamii kwenye halmashauri hiyo ikiwemo masuala ya elimu la TUVAMO kupitia mradi huo wa ‘Rudisha Msichana Shule’ ambapo mwaka huu 2024 unatekelezwa kwa kipindi cha tatu cha mradi kwenye kata tatu wilayani humo ikiwemo Ziwani, Nanguruwe na Moma.

Mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miezi sita sita kupitia ufadhili wa Shirika la kitanzania la Women Fund Tanzania Trust (WFT)lililopo Jijini Dar es salaam.
Uliyoanzishwa baada ya kugundua uwepo wa changamoto kwa baadhi ya jamii kutoona umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike na watoto wenyewe kusitisha masomo hivyo wakaona ipo haja ya kuanzisha mradi utaosaidia vijana hasa wa kike waliyositisha masomo waweze kurejea shule.
‘’Tulipofatilia takwimu zilionyesha kati ya wanafunzi wa kiume na wa kike, wanafunzi wa kike wanaacha sana shule kutokana na changamoto ya ujauzito, utoro, mimba za utotoni,”amesema Mpinga
Ameongeza kuwa “Tukaona kuna haja ya kuwapa hamasa mabinti ili waweze kurejea tena shule, na mradi ni wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2022 hadi mwaka huu 2024 na tunatekeleza kwa kipindi cha miezi sita sita’’
Aidha awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi mwaka 2022 hadi 2023 walifanikiwa kufanya uhamasishaji katika kata nne wilayani humo ikiwemo Nanguruwe, Ziwani, Moma na Mbawala.

Hata hivyo walifanikisha kuwafikia wasichana 120 kutoka katika shule za msingi na sekondari kwenye kata hizo hawakubahatika kupata msichana hata mmoja mwenye utayari wa kurejea shule kwa madai ya kuwa wazazi kukosa ushiriki wa moja kwa moja katika jitihada hizo.
Hata hivyo hawakuishia hapo tu bali waliendelea na uhamasishaji kupitia mikutano ya vijiji kwa kushirikiana na serikali na wazazi ndani ya kata hizo na awamu hii ya tatu ya mradi mwaka 2024 unatekelezwa kwenye kata tatu.
Kata hizo ikiwemo Ziwani, Nanguruwe na Moma wamefanikiwa kupata wasichana 10 waliyoonyesha nia ya kurejea tena shuleni na tayari wako shuleni wanaendelea na masomo.
‘’Lengo letu lilikuwa kuwapeleka wasichana hawa kwenye mfumo rasmi wa elimu kwenye zile shule walizokuwa wakisoma awali lakini kutokana na uwepo wa baadhi ya changamoto za utekelezaji tukashindwa kuwarudisha kwa wakati shule na badala yake tumewarudisha kwenye elimu haina mwisho katika chuo cha maendeleo ya wananchi cha Mtawanya (FDC) Mtwara na wanaendelea na masomo’’
Baadhi ya wazazi kwenye mafunzo hayo akiwemo Asha Saidi kutoka kata ya Nanguruwe ambaye mtoto wake amehamasika kurejea tena shuleni katika shule hiyo ya Mtawanya, amefurahishwa na kitendo cha mtoto wake kurejea tena shule huku akipongeza jitihada zilizofanywa na shirika hilo kwa kuendelea kuwahamasisha wazazi kutambua na kuona umuhimu wa elimu.
Mzazi kutoka kata ya Moma ambaye bado mtoto wake hajarejea shule, Ahmad Salum amesema kwa sasa amehamasika na atahakikisha mtoto wake anarejea shule baada ya shirika hilo kuwapatia elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto kwani uridhi mkubwa katika maisha ni elimu.
Nae Mwanafunzi ambaye alisitisha shule na sasa amerejea tena shule kwenye shule hiyo ya Mtawanya, Pili Ramadhani kutoka wenye kata hiyo ya Nanguruwe ‘’Nimefurahi sana kurudishwa shule kuendelea na masomo naahidi kusoma kwa bidii na wanawahamasisha wasichana wenzangu ambao bado hawajafanya maamuzi ya kurejea tena shule warudi ili tusome tufikie ndoto zetu’’
Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Moma, Mbalu Sylivester amepongeza uwepo wa maradi kwani baadhi ya watoto waliyokuwa hawaendi shule kwenye maeneo yao sasa wanaenda na maendeleo yao ni mazuri na kuwasisitiza wazazi hao kuwa, watambue umuhimu wa elimu kwasababu elimu ndiyo kila kitu katika maisha.



