Wazee Dar wapinga uchochezi uchaguzi mkuu

DAR ES SALAAM: WAZEE wa jiji la Dar es Salaam wanapinga kauli za kuhamasisha wananchi kususia uchaguzi, wakisisitiza kuwa maneno hayo hayana tija na yanahatarisha mshikamano wa taifa.

Mkurugenzi wa Shirika la Vijana na Wanawake (TAFEYOCO), Elvis Makumbo, amsema kuna watu wanaojificha kwenye mwamvuli wa uzalendo lakini ajenda yao ni kutafuta viongozi watakaowapa manufaa binafsi.

“Tusifate maneno ya wenye uchu wa madaraka. Tulipata uhuru kwa njia ya amani, basi tuwachague viongozi kwa amani kwa kufuata utaratibu wa nchi,” amesema.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Ushauri Mtaa wa Jogoo, Romald Rwechungura, anasisitiza kuwa wazee hawawezi kukaa kimya mbele ya wito wa kususia uchaguzi. “Wazee tukinyamaza ni sawa na kuridhia jambo lisilofaa. Tunataka vijana wetu washiriki na kuimarisha demokrasia,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Kata ya Goba, Yahaya Mjema, anakumbusha kuwa amani ni urithi uliotengenezwa tangu enzi za uhuru.

“Hatuna tofauti ya dini wala kabila. Tunaliomba Jeshi la Polisi liwe na hekima na subira kukabiliana na changamoto za uvunjifu wa amani,” amesema. Katibu wa Kikundi cha Uwazi kilichopo Mbezi Luis, Ahmad Tamla, anaongeza kuwa wazee wanapaswa kupewa nafasi zaidi kwenye ngazi za maamuzi.

“Elimu ya siasa iliyokuwa inafundisha uzalendo irudi. Uchaguzi utafanyika, na sisi wazee tunasisitiza tutii mamlaka ya nchi kwa mujibu wa katiba na sheria,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button