Waziri Mkuu atoa maelekezo uendeshaji SGR

DODOMA: WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Uchukuzi iendelee kulisimamia kwa karibu Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kuhakikisha huduma za treni ya SGR zinaboreshwa na miundombinu inaimarishwa ili mradi huo udumu.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati wa kuahirisha Mkutano wa 16 wa Bunge, Majaliwa amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali itaendeleza sekta ya uchukuzi ambapo pamoja na mambo mengine itasimamia sekta ya reli ikiwemo ujenzi wa SGR na uendeshaji wa treni ya kisasa ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

Majaliwa amesema kuwa Desemba 31, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza kuanza uendeshaji wa reli ya SGR kwa kipande cha Dar es Salaam – Dodoma ifikapo mwezi Julai, 2024.

“Naomba kulitaarifu bunge lako tukufu kuwa, safari za treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam – Morogoro zilianza tarehe 14 Juni 2024 na tarehe 25 Julai 2024 uendeshaji wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ulianza,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema Agosti 10, 2024 , Rais Samia Suluhu Hassan alizindua utoaji wa huduma za reli ya kisasa ya SGR kutoka jiji la Dar es salaam kupitia Mkoa wa Morogoro hadi Dodoma.

SOMA: Serikali yataja mikakati kuwalinda wenye ualbino

Amesema treni hiyo inaendelea kutoa huduma kwa wananchi na imechangia kuimarisha sekta ya usafirishaji. “Kipekee ninaomba kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia maono yake na kwa kweli anaahidi, anatekeleza, Kazi Iendelee”.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo isimamie kwa ukaribu upatikanaji na usambazi wa pembejeo za kilimo hususani mbolea ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa kilimo na kwa kuzingatia jiografia za kanda za kilimo nchini.

Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa maofisa ugani kwa kuwataka waendelee kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya teknolojia bora za uhifadhi wa mazao ya chakula na matumizi sahihi ya chakula hicho katika ngazi ya familia.

Habari Zifananazo

Back to top button