Waziri Mkuu wa zamani ahukumiwa miaka 5 jela

MAHAKAMA maalumu nchini Guinea imemhukumu Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Ibrahima Kassory Fofana kifungo cha miaka mitano jela baada ya kumkuta na hatia ya kuhusika na ufisadi pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Ibrahima Kassory Fofana aliyewahi kuwa Waziri Mkuu chini ya Serikali ya Rais Alpha Conde, pia alitozwa faini ya Faranga bilioni 2 ambazo ni sawa na Dola 230,000 na Mahakama hiyo mjini Conakry kwa kosa hilo.
Fofana amekutwa na hatia ya kutumia vibaya fedha za umma Faranga bilioni 15 ambazo zilitengwa kwa ajili ya miradi ya shughuli za ustawi wa jamii, ikiwemo wakati wa janga la Corona katika serikali iliyopita.
Waziri mkuu huyo wa zamani wa Guinea ni mmoja kati ya maofisa wengi wa serikali hiyo iliyoondolewa madarakani na kushitakiwa na kuhukumiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi na makosa mengine ya uporaji fedha katika mahakama maalumu iliyoundwa baada ya utawala wa kijeshi nchini humo kutwaa madaraka.



