‘Wekeni mikakati wanafunzi waifahamu jiosayansi’

MBEYA: Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Zena Ahmed, ametoa wito kwa wataalamu wa jiosayansi nchini kuanza mikakati madhubuti ya kutoa elimu na kuhamasisha wanafunzi kuifahamu na kuipenda fani hiyo ili kuongeza idadi ya wataalamu.

Amesema licha ya umuhimu mkubwa wa jiosayansi katika maendeleo ya taifa, bado uelewa wake miongoni mwa wananchi na wanafunzi ni mdogo na kwamba kukosekana uelewa huo kumekuwa chanzo cha idadi ndogo ya wataalamu wa jiosayansi nchini.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa Jumuiya ya Wanajiosayansi Tanzania (TGS) unaofanyika jijini Mbeya, Mhandisi Zena amesema jiosayansi ina mchango muhimu katika sekta nyingi ikiwemo kilimo, ujenzi na maendeleo ya miundombinu, lakini wengi hawafahamu umuhimu huo.

Amesisitiza kuwa wataalamu hao wanapaswa kutumia vyombo vya habari kutoa elimu kwa umma kuhusu maana ya fani ya jiosayansi, faida zake na namna inavyoweza kuchangia ustawi wa jamii kupitia sekta mbalimbali.

Mhandisi Zena amefafanua kuwa fani ya jiosayansi inaweza kumsaidia mkulima kuboresha kilimo kupitia uelewa wa udongo na maji, lakini pia inaweza kusaidia wakandarasi kujenga kwa usahihi na usalama, akieleza kuwa kukosekana kwa matumizi ya utaalamu huo kumesababisha changamoto kwenye ujenzi wa baadhi ya miundombinu ya ujenzi na maji.

Ameeleza kuwa sekta ya jiosayansi ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050 kupitia usimamizi na utambuzi wa rasilimali muhimu za nishati kama gesi asilia, jotoardhi, makaa ya mawe na madini ya urani yanayotumika katika uzalishaji wa umeme.

Katika hatua nyingine, ameahidi kuwa serikali itaharakisha mchakato wa kuanzisha Bodi ya Uthibiti wa Fani ya Jiosayansi ili kuhakikisha kuwa kazi za kitaalamu zinafanywa na wataalamu waliothibitishwa akieleza kuwa kukosekana kwa bodi kunatoa mianya kwa watu wasio na sifa kufanya kazi za kitaalamu na kuhatarisha hadhi ya fani hiyo.

 

Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya ya Wanajiosayansi Tanzania (TGS), Profesa Elisante Mshiu, amesema zaidi ya wanachama 4,000 kutoka vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi wanashiriki mkutano huo.

Amesema lengo kuu ni kubadilishana uzoefu, kujadili teknolojia mpya na kutoa taarifa muhimu kwa ajili ya kuboresha sekta ya jiosayansi nchini, huku akiomba Serikali kuwatumia wanataaluma hao katika kufanikisha malengo ya Dira 2050.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button