Wenye ulemavu wapewa mikono ya bandia bure

ARUSHA: SERIKALI kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo nchini kupitia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru imewapatia wananchi wenye ulemavu mikono ya bandia bure.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa zoezi hilo, Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Mount Meru Dk, Kipapi Mlambo amewataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwani fursa hizo zinatokea kwa nadra.
“Huduma hii inatolewa bure lakini sio kwamba ni bure kabisa bali Kuna watu wamegharamika na kujitolea na tulipofanya hesabu ya gharama za huduma hii ya mkono mmoja ni karibu milioni nne za kitanzania, kwa maisha ya kawaida sio rahisi kuzipata na hivyo kwa nyinyi ambao mmepata hii fursa mkawatangazie wengine ili waje wahudumiwe,” amesema Dk Kipapi Mlambo.

Pia Dk Kipapi amewashukuru wadau hao kwa kuonyesha ushirikiano na Serikali katika kufanikisha zoezi hilo ambalo linawagusa maisha ya Watanzania walio wengi.
Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru, Daniel Kasikiwe amewata wananchi wanaopata huduma ya mikono ya bandia bure kuitunza kwa sababu imetumia zaidi ya milioni nne kwa mkono mmoja.




