Wenyeviti wa mitaa hakikisheni wananchi wanapiga kura kwa amani-RC Makalla
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla leo Oktoba 24, 2025 amekutana na Wenyeviti na Watendaji wa serikali za Mitaa Jiji la Arusha, akiwataka kutimiza majukumu yao kikamilifu katika kuhakikisha kila Mwananchi mwenye sifa anapata fursa ya kushiriki vyema kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa kuhakikishiwa usalama na mazingira tulivu wakati wa uchaguzi Mkuu.
“Mkoa huu ni Mkoa Mkubwa, ni mkoa wenye uchumi unaotegemea Kilimo, biashara na utalii. Ahadi yangu kwenu, amani haina mjadala na ni kipaumbele cha kwanza kwani ili tuendelee kufanya shughuli zetu zote ikiwemo biashara na Utalii msingi wake ni amani na utulivu, Wito wangu kwenu ni kuhakikisha amani hiyo tunailinda kwa wivu mkubwa na Wivu huo ninyi wote mmepewa dhamana katika maeneo yenu kuhakikisha wananchi wenu wanakuwa salama,” amesisitiza CPA Makalla.
Aidha Katika Mkutano huo CPA Makalla pia amewahakikishia wananchi wote wa Mkoa wa Arusha amani, usalama na utulivu hapo Oktoba 29, akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kushiriki kwenye zoezi hilo la Kikatiba.
Mapema leo kulingana na taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Moses Kusiluka kwa Vyombo vya habari, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameidhinisha Jumatano ya Oktoba 29, 2025 kuwa siku ya mapumziko Kitaifa ili kutoa fursa kwa watumishi wa umma na wafanyakazi kuweza kushiriki kikamilifu kwenye Upigaji wa kura kwa kuwachagua Madiwani, Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watakaoongoza kwa miaka mitano ijayo.



