WRM wajivunia kusaidia maendeleo ya jamii

ILALA, Dar es Salaam: KANISA la The Word of Reconciliation Ministries (WRM), linaadhimisha miaka 17 ya huduma tangu kuanzishwa kwake, huku likijivunia ushiriki wake katika kusaidia maendeleo ya kijamii.

Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika Aprili mosi, 2024 katika kanisa hilo, lililopo Kivule-Matembele ya Pili, Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Ardhi, Jerry Silaa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Nabii Nicolaus Suguye amesema wamekuwa karibu na jamii kwa kutoa misaada mbalimbali ikiwamo kwa wajane na watoto yatima.

Advertisement

Nabii Suguye amesema mbali na huduma za kiroho pia wameshiriki katika kuvuta umeme na kusapoti ujenzi wa ukuta wa shule ya Kivule na kutoa vifaa tiba kwenye Hospitali ya Kivule.

“Tumekuwa karibu sana na jamii kwa kurudisha kwao kile tunachopata, na huu ndio utamaduni wetu sisi watu wa mungu lengo ni kuhubiri injili na kuilingania jamii kuwa katika maadili mazuri,” amesema Suguye.

Kuhusu changamoto kanisa hilo ilizopitia katika kipindi chote cha miaka 17, Nabii huyo alisema hazijawarudisha nyuma wala kuyumba bali zimewajenga zaidi kiimani.

Alisema pamoja na huduma za maombezi zitakazokuwepo siku hiyo, pia kutakuwa na burudani kutoka kwa waimbaji mbalimbali wa nyimbo za injili na wachekeshaji wanaoigiza sauti za viongozi.

“Tunawakaribisha waumini na watu mbalimbali sababu siku hiyo itakuwa ni siku ya furaha kutakuwa na chakula cha kila aina, ambacho kitapatikana bure kwa kila atakayehudhuria na usafiri wa bure utaanzia maeneo ya Banana,” amesema Nabii Suguye.