Yaliyojiri Mkutano wa Kwanza Bunge la 13

WIKI iliyopita, naweza kusema ilikuwa Wiki ya Bunge la 13 tangu Novemba 8 hadi 14, 2025.

Katika kipindi hicho, wabunge ambao ni matunda ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 29, 2025 wanaanza kwa kuitikia mwito wa Ofisi ya Bunge kuwasili Dodoma kujisajili na kufanya shughuli mbalimbali za kiutawala kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 13, Novemba 11, mwaka huu.

Kama lilivyosema Tangazo la Rais katika Gazeti la Serikali Toleo Maalumu Na. 11 la Novemba 4, 2025, Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 13, Kikao cha Kwanza ukafanyika Novemba 11, mwaka huu baada ya kukamilika kwa usajili.

SOMA: Rais Samia afungua Bunge 13

Awali, tangazo hilo lilitaja shughuli za Mkutano wa Kwanza wa Bunge hili kuwa ni pamoja Uchaguzi wa Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Siku hiyo, wabunge wote wanapiga kura na kumchagua Spika ambaye sasa amerithi mikoba ya Dk Tulia Ackson ambaye alikuwa Spika wa Bunge la 12.

Kura zao zinaamua aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge lililopita na Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Azan Zungu awe Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nafasi ya Spika wa Bunge ambayo kabla ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 ilikuwa ikishikiliwa na Zungu, baadaye nayo ikapata mtu kwa wabunge ‘kumwaga’ kura zao kwa Daniel Silo.

Baada ya kumchagua Zungu kuwa spika na kuapishwa, anawaapisha wabunge mmoja baada mwingine; wanaapa kiapo cha uaminifu. Kisha bunge kwa umoja wake, linafikwa na jukumu lingine la kikatiba la kuthibitisha uteuzi wa waziri mkuu.

Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba.

Novemba 13, 2025, jina la waziri mkuu mteule linawasilishwa kwa spika bungeni na ‘mpambe wa rais.’ Kisha, Spika Zungu anatengua kitendawili kilichosubiriwa kwa hamu na Watanzania. Anataja jina la Dk Mwigulu Lameck Nchemba kuwa ndiye aliyeteuliwa na Rais kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wabunge wanathibitisha uteuzi wa Mwigulu kuwa Waziri Mkuu kwa kura 369 kati ya kura 371 zilizopigwa. Mwigulu ambaye amekuwa Mbunge wa Iramba Magharibi tangu mwaka 2010, amewahi kushika nafasi mbalimbali serikalini zikiwemo za Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Kilimo, Waziri wa Mambo ya Ndani na hata nafasi ya mwisho ya Waziri wa Fedha kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu.

Akizungumza baada ya kupigiwa kura za kumthibitisha kuwa Waziri Mkuu, Mwigulu anaonesha kuyafahamu na kukerwa na maisha ya umaskini. Anasema suala la umaskini analifahamu si kwa kulisoma katika vitabu, bali kwa kuwa ameishi maisha ya umaskini kwa takribani miaka 32.

Mwigulu anasema: “Natambua hali ya umaskini uliopo nchini kwa sababu nimeishi na hali hiyo kwa zaidi ya miaka 32; natambua changamoto ya ajira kwa vijana nchini, natambua ugumu wa maisha uliopo.”

Kisha anaonya watumishi wa umma wazembe, wala rushwa na wenye lugha chafu akisisitiza kuwa, wanapaswa kujirekebisha kwani hawatakuwa na nafasi. Novemba 14, mwaka huu, mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Chamwino Dodoma, Mwigulu anaapa kuitumikia Tanzania.

Ndipo Rais Samia anasema katika hafla hiyo ya uapisho kuwa, uteuzi huo umezingatia mambo mbalimbali yaliyochunguzwa kwa maslahi ya taifa. Anamtaka waziri mkuu mpya kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, ili ahadi zilizotolewa kwa wananchi zitekelezwe kama ilivyopangwa.

Mkuu wa nchi anamhimiza waziri mkuu huyo kuwa mwangalifu dhidi ya vishawishi vinavyoweza kujitokeza wakati wa akitekeleza majukumu yake kwa kuwa jukumu (cheo) alilopewa ni kubwa.

Hafla hiyo ya uapisho inahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT), Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), viongozi wa siasa, viongozi wa dini na wadau wengine. Siku hiyo hiyo jioni, itifaki zote zinazingatiwa ukiwamo ukaguzi wa gwaride katika viwanja vya Bunge. Kisha, rais anaingia bungeni.

Ikumbukwe kuwa, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bunge lina sehemu mbili ambazo ni wajumbe wa aina zote yaani, wabunge wa kuchaguliwa katika majimbo, wabunge wa viti maalumu, wanasheria wa serikali, wabunge wa kuteuliwa na rais na spika (kama si mbunge).

Spika wa Bunge, Musa Azan Zungu.

Ibara ya 63 (1) inamtaja rais kama sehemu moja ya bunge kikisema: “Atatekeleza madaraka yote aliyokabidhiwa na katiba hii kwa ajili hiyo.” Ndipo Rais Samia anahutubia Bunge na wananchi kwa ujumla na kutamka rasmi. Miongoni mwa mambo anayosema rais katika hotuba yake ya uzinduzi wa bunge kabla ya kutamka rasmi uzinduzi, ni pamoja na maridhiano.

Anaanza: “Kwa mujibu wa Ibara ya 91 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana dhima ya kulifungua rasmi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Anasema: “Ilani ya CCM ya 2025-2030 imeahidi na mimi nilitangaza ahadi hiyo kuwa nitaunda Tume ya kuanzisha ‘mazungumzo’ ya ‘maridhiano’ na ‘upatanishi’ na kuandaa mazingira ya kuanza kwa mchakato wa mabadiliko ya katiba.”

“Hata hivyo, kutokana na uvunjifu wa amani uliotokea nchini, tunahitaji kufanya tathmini ya kina ili tujue kiini na sababu ya kadhia hiyo ndipo tuunde Tume ya Maridhiano,” anasema Samia. Anaongeza: “Katika muhula kwa kwanza wa Awamu ya Sita tulikuja na Falsafa ya ‘R4’ (Maridhiano- ‘Reconciliation’, Ujenzi mpya wa taifa- ‘Rebuliding’, Ustahimilivu- ‘Resilience’ na Mageuzi – ‘Reform’) ili kuliunganisha taifa.”

“Serikali ilionesha utayari wakati wote kuleta maridhiano ili kwa pamoja tuweze kulijenga na kulitunza Taifa letu,” anasema. Anaongeza: “Serikali ilinyoosha mkono kuwavuta na kuwakaribisha vyama vya siasa, vyama vya kijamii, sekta binafsi na hata jumuiya za kimataifa, ili kwa pamoja tuijenge Tanzania.”

Rais Samia anafafanua bungeni: “Waheshimiwa Wabunge, mkono huo wa urahimu ulileta matumaini kwa nchi, kabla ya baadhi ya wadau kuamua kuuachilia au kuuputa mkono huo. Kwa kuwa wananchi wa Tanzania wamenipa ridhaa ya kuendelea kuiongoza nchi hii, sitachoka kunyoosha tena mkono wa maridhiano.”

“Ni matumaini yangu kuwa, wadau wa kisiasa wataupokea kwa dhati mkono wa maelewano, ili kwa pamoja tujenge mazingira mwafaka kwa maendeleo ya taifa letu. Tutajifunza kutokana na makosa na mapungufu ya taasisi zetu za kidemokrasia,” anaeleza.

Kwa mujibu wa mkuu wa nchi huyo, Tanzania ina uzoefu wa miongo mingi ya demokrasia na amani. “Tanzania ina demokrasia iliyokomaa hata hivyo, tutaendelea kuiboresha kulingana na mazingira na wakati. Ni jukumu letu sasa kujielekeza kwenye maboresho hayo kwa utashi wetu bila shinikizo lolote,” anasema.

Kipekee, Rais Samia anaongeza: “Mheshimiwa Spika! Naliahidi Bunge lako Tukufu ushirikiano wangu binafsi na wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuyatekeleza yote haya kwa manufaa ya Watanzania ambao Wabunge hawa wanawawakilisha.”

“Rai yangu kwenu ni kutoa ushirikiano wa dhati kwa Serikali. Kwa pamoja, tutajenga nchi ambayo mifumo inafanya kazi na miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi ili Watanzania nao waweze kufanya kazi zao kwa bidii na weledi kwa maendeleo ya taifa letu,” anasema.

Anaongeza: “Namuomba Mwenyezi Mungu kuwa, mwisho wa utumishi wa Awamu ya Sita usipimwe tu kwa vitu vitakavyoachwa, bali pia kwa tabasamu la utu litakaloachwa kwenye nyuso za Watanzania.” Katika kuhitimisha hotuba yake bungeni, Rais Samia anasema, “Baada ya kusema hayo, sasa ninayo heshima ya kutamka kwamba ‘Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa limefunguliwa rasmi. Mungu Ibariki Afrika!

Mungu Ibariki Tanzania! Mungu libariki Bunge letu na Wabunge wake!” Kisha katika nafasi tofauti Spika Zungu na Waziri Mkuu, Mwigulu wanasema Mkutano wa Pili wa Bunge la 13 utafanyika Januari 27, 2026.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button