10 mbaroni tuhuma uvamizi nyumba, kujeruhi watano

Atuhumiwa kumbaka ajuza wa miaka 80

WATU zaidi ya 10 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Pwani kwa tuhuma za kuvamia nyumba wakiwa na silaha za jadi na kujeruhi watu watano.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani (ACP), Pius Lutumo alisema kuwa watu waliojeruhiwa walipatiwa huduma na kuruhusiwa kurudi nyumbani huku mmoja akihamishiwa Hospitali ya Mloganzila.

Lutumo alisema kuwa watu waliovamia walitumia silaha ikiwa ni pamoja na marungu na mapanga ambapo hata hivyo walikurupushwa na kushindwa kuiba kitu chochote.

Advertisement

“Kwenye tukio hilo watu watano walijeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi kwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani huku majeruhi mmoja akihamishiwa hospitali ya Mloganzila kwa matibabu zaidi,” alisema Lutumo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Ungindoni Kata ya Kongowe wilayani Kibaha, Zuberi Mmula alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi Novemba 15 majira ya saa 9 usiku karibu na Msikiti.

Mmula alisema kuwa alipigiwa simu majira ya saa 9 usiku kutaarifiwa tukio hilo ambapo aliwasiliana na polisi ambao walikuwa doria na walipofika vijana waliotekeleza tukio hilo walikimbia.

Alisema kuwa vijana hao walivamia nyumba tatu ambapo waliwajeruhi wanafunzi wanaosoma chuo cha ufundi cha Veta Kongowe ambao wamepanga jirani na chuo hicho.

“Tunawashukuru askari kwa kuwahi kufika kwenye eneo la tukio lakini kwa bahati mbaya vijana hao walikimbia na tunaamini watakamatwa kwani Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo,” alisema Mmula.

Kwa upande wa mmoja wa wananchi ambaye nyumba yake ilivamiwa na vijana hao, Erasto Mbwambo alisema kuwa vijana wake wawili walijeruhiwa.

Mbwambo alisema kuwa wakati tukio linatokea hakuwepo alipewa taarifa na kufika asubuhi na kuwakuta vijana wake wakiwa wamejeruhiwa na kuwapeleka Tumbi kwa matibabu.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *