10 wanusurika kifo kwa kushambuliwa na fisi Geita

WATU 10 ikiwemo watano wa familia moja katika kijiji cha Nyamarimbe, kata ya Nyamarimbe Tarafa ya Busanda wilayani Geita wamenusurika kufa baada ya kushambuliwa na fisi mmoja kijijini hapo.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Berthaneema Mlay amethibitisha alipozungumza na waandishi na kueleza tukio limetokea jioni Machi 29, 2023.

Advertisement

ACP Berthaneema amesema kabla ya kufanya shambulizi hilo, watoto wawili walinusurika kushambuliwa na fisi huyo wakiwa machungani ambapo walikimbia kutoa taarifa na fisi huyo kuua ng’ombe mmoja.

“Waliojeruhiwa ni 10 ambao walipata huduma ya kwanza katika kituo cha afya cha Nyamarimbe, na baadaye walihamishiwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Geita kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Wananchi watano ni watu wa familia moja kwa maana kwamba kuna mama na watoto wake wawili wa kike na mmoja wa kiume pamoja na kaka yake.” Amesema Kamanda na kuongeza;

“Baada ya wananchi kupata taarifa wakawa wamekuja, yule fisi alitoka kule vichakani baada ya kusikia sauti za watu, akaanza kuvamia wale wananchi.

Kamanda Berthaneema amesema askari wa vituo vidogo vya polisi karibu na eneo la tukio waliagizwa kwenda kukabiliana na fisi huyo ambapo walimushambulia na kufanikiwa kumuua kwa risasi tatu.