Buruhani aomba uchunguzi tuhuma za rushwa UVCCM

DODOMA: KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Faris Buruhani, amekiomba Chama hicho kuchunguza tuhuma za rushwa zinazodaiwa kuwakabili baadhi ya vijana ili ukweli ubainike na haki itendeke.

Buruhani ametoa ombi hilo leo Oktoba 19, 2026 jijini Dodoma alipozungumza na vijana waliojitokeza kumpokea katika Ofisi za Makao Makuu ya UVCCM, kufuatia uteuzi wake kushika nafasi hiyo.

Amesema uchunguzi huo unapaswa kufanyika kwa kuzingatia Katiba, kanuni na taratibu za chama, huku hatua stahiki zikichukuliwa iwapo tuhuma hizo zitathibitika.

“Kama kweli tuhuma hizo zina ukweli, basi hatua zichukuliwe kwa mujibu wa utaratibu. Vilevile, kama tuhuma hizo hazina ukweli, hatua zichukuliwe kwa mujibu wa taratibu za chama,” amesema.

Buruhani pia amesisitiza umuhimu wa vijana kulinda maslahi ya taifa, akisema Tanzania ni urithi walioachiwa na wazee wao katika hali ya amani, usalama na utulivu.

Amesema kila kizazi kina wajibu wa kuhakikisha amani na utulivu huo vinaendelea kulindwa, akiwataka vijana kuweka mbele maslahi ya taifa wakati wa kujadili masuala ya kitaifa.

“Masuala ya kitaifa yanapojadiliwa, vijana wanapaswa kuweka mbele maslahi ya nchi badala ya tofauti za kisiasa ili kudumisha amani na mshikamano,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Bara, Mussa Mwakitinya, amesema ujio wa Buruhani katika nafasi hiyo unaungwa mkono na vijana, akiahidi kuendelea kushirikiana naye katika kuimarisha shughuli za jumuiya.

Mwakitinya amesema uteuzi huo umeweka matarajio makubwa kwa vijana, akimtaka Buruhani kutumia nafasi hiyo kuendeleza ujenzi wa CCM na kuimarisha ushiriki wa vijana katika shughuli za chama.

Naye, Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa UVCCM Mkoa wa Katavi na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini vijana na kuwapa nafasi za uongozi.

Luswetula amesema yuko tayari kumpa Buruhani ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake na kuimarisha shughuli za UVCCM.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button