Uholanzi yamtunuku Melo tuzo haki za binadamu

DAR ES SALAAM: UBALOZI wa Uholanzi nchini Tanzania umemtangaza Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiAfrica, Maxence Melo, kuwa mshindi wa tuzo ya haki za binadamu ya Embassy Tulip Award 2026, akitambuliwa kwa mchango wake katika kutetea uhuru wa kujieleza, kulinda taarifa za vyanzo vya habari na kuimarisha uwajibikaji kupitia majukwaa ya kidijitali.

Mshindi huyo ameingia pia katika orodha ya washiriki watano waliofuzu hatua ya mwisho ya tuzo ya kimataifa ya Central Human Rights Tulip, itakayotolewa Desemba 17, mwaka huu, mjini The Hague, Uholanzi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Novemba 17, 2026, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Marjo Crompvoets, amesema Melo amechaguliwa kutokana na mchango wake katika kuendeleza haki za binadamu kupitia teknolojia, ubunifu na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika masuala ya utawala na uwajibikaji.

Amesema tuzo hiyo inalenga kutambua ujasiri, kujitolea na matokeo ya kazi za watu binafsi, taasisi, mitandao na harakati zinazohusika katika kukuza na kulinda haki za binadamu katika nchi zao.

Amesema kwa mwaka huu, ubalozi ulipokea jumla ya mapendekezo 28 kutoka kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo watu 21 walipendekezwa na wengine saba walijipendekeza wenyewe.

Ameeleza kuwa mchakato wa kumpata mshindi ulisimamiwa na kamati huru ya uchaguzi iliyoundwa na wajumbe wanne, wakiwemo wafanyakazi wawili wa ubalozi na watetezi wawili wa haki za binadamu kutoka nje ya taasisi hiyo ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru na bila upendeleo.

Aidha, amesema mchango wa Melo hauishii katika kulinda uhuru wa kujieleza, bali pia umechangia katika maboresho ya sera na sheria nchini, akitolea mfano ushiriki wake katika muungano wa wadau wa serikali na wasiokuwa wa serikali ulioandaa muswada wa mfano kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi.

Ameongeza kuwa JamiiAfrica imeanzisha mifumo mbalimbali ya kidijitali inayolenga kuimarisha uwajibikaji, ikiwemo FichuaUovu inayowezesha wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa usiri, Kero kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko kuhusu huduma za umma na JamiiCheck inayotumia teknolojia ya akili mnemba (AI) kusaidia uhakiki wa taarifa.

Katika hatua nyingine, Crompvoets amesema washindi wa tuzo za Embassy Tulip Award kutoka nchi mbalimbali hupata zawadi ya fedha za Euro 5,000 kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za utetezi wa haki za binadamu, sanamu ya shaba yenye umbo la ua la tulip, kutambuliwa rasmi, mafunzo ya uandishi wa habari na usimulizi wa habari pamoja na fursa za kujenga mitandao ya kimataifa.

Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Ubalozi wa Uholanzi, Chikulupi Kasaka, amesema tuzo hiyo inalenga kutambua na kuenzi watu wanaotoa mchango mkubwa katika kulinda na kutetea haki za binadamu.

Kasaka amesema tuzo hiyo ilianza kutolewa na ubalozi huo nchini Tanzania mwaka 2025, huku mwaka huu ikiwa ni mara ya pili kuandaliwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button