13 mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya wafugaji
WATU 13 akiwemo Mtemi wa Jeshi la Jadi maarufu Sungusungu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora kwa tuhuma ya mauaji ya wafugaji watatu wa Kata ya Isakamaliwa wilayani Igunga.
Mwendesha mashitaka wa Polisi Wilaya ya Igunga, Elimajid Kweyamba aliwataja washitakiwa mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Igunga, Ridia Ilunda mshitakiwa wa kwanza ni Jijadi Katambi (43) ambaye ni Mtemi wa Sungusungu Kata ya Isakamaliwa.
Watu wengine waliofikishwa mahakamani hapo ni Maleba Machenge (37), Ngoga Ifegelo (50), Ndulu Manyenye (32), Shakali Ifegelo (30), Magembe Mwandu (25), Mahona Jilala (35), Bakari Hamis (45), Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Isakamaliwa, Shija Mboje (48) na Mwalimu wa Shule ya Msingi Isakamaliwa, Michael Masanja (36).
Wengine ni Kulala Shigela (38), Masunga Kulwa (39) na Nkwabi Mipawa (58) wote wakazi wa Kata ya Isakamaliwa.
Elimajid alisema mashitaka ya kwanza yanayowakabili washitakiwa hao ni kwamba Mei 12, 2022 majira ya saa 8:00 mchana katika Kijiji cha Isakamaliwa na Kata ya Isakamaliwa wakiwa na nia ovu walimuua Darushi Bukwere (26) mkazi wa Kata ya Isakamaliwa.
Katika mashitaka ya pili washitakiwa hao katika tarehe hiyo na muda huo katika kata hiyo ya Isakamaliwa wakiwa na nia ovu walimuua, Gwisu Manyenye (30) mkazi wa Kijiji cha Isakamaliwa.
Aliiambia mahakama kuwa katika mashitaka ya tatu yanayowakabili washitakiwa ni kwamba katika tarehe hiyo na muda huo washitakiwa wote kwa pamoja walimuua Jacob Tungu (32) mkazi wa Kata ya Isakamaliwa.
Mwendesha mashitaka aliiambia mahakama kuwa washitakiwa wote walitenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 196 kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2019.
Hata hivyo, baada ya kusomewa mashitaka hayo matatu washitakiwa wote hawakutakiwa kujibu kitu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 30 mwaka huu itakapotajwa tena na washitakiwa wote wamepelekwa mahabusu.