WATU 35 wamefariki na wengine 14 wameokolewa baada ya kutumbukia kwenye kisima walipokuwa wakisali kwenye hekalu moja katika jimbo la kati la India la Madhya Pradesh.
Ajali hiyo ilitokea jana Alhamisi wakati wa hafla ya maombi iliyoandaliwa katika hekalu la Beleshwar Mahadev Jhulelal kwenye hafla ya sherehe ya Kihindu ya Ram Navami.
Umati mkubwa wa waumini walikuwa wamesimama kwenye slab ya zege iliyofunika kisima ambacho kiliporomoka kutokana uzito wao na kuwatumbukiza watu wengi kwenye kisima chenye kina cha futi 40 (12m).
Vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti kwamba hekalu hilo lilijengwa baada ya kisima hicho kufunikwa takriban miongo minne iliyopita.
Afisa mkuu Illayaraja T aliambia kituo cha habari cha ANI kuwa watu 18 walilazwa katika hospitali hiyo baada ya kuokolewa na watu wawili wameruhusiwa kufikia sasa. Aliongeza kuwa msako bado unaendelea ili kumpata mtu aliyetoweka.
Timu ya wafanyakazi 75, ikiwa ni pamoja na wale wa serikali na vikosi vya kitaifa vya kukabiliana na maafa wanashiriki katika juhudi za uokoaji.
Waziri Mkuu Shivraj Singh Chouhan ametangaza fidia ya rupia 500,000 ($6,000; £4,900) kwa jamaa za marehemu na rupia 50,000 kwa waliojeruhiwa.
Modi alituma salamu zake za rambirambi kwa familia za waathiriwa na pia kutangaza fidia ya rupia 200,000 kwao.