41 watengenezwa mishipa kuchuja damu Mloganzila

DAR ES SALAAM: JUMLA ya watu 41 wamefanyiwa upasuaji wa kutengeneza mishipa ya kuchuja damu na wanne kupandikizwa figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.

Kwa idadi hiyo ya wagonjwa waliohudumiwa Mloganzila imeweka rekodi mpya kwa kuwa hospitali ya kwanza nchini kufanya huduma za kutengeneza mishipa ya kuchuja damu kwa wakati mmoja.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili,Dk Delila Kimambo amesema kambi hiyo ya matibabu ilianza Julai 20 hadi 23 ,2025 ambapo idadi hiyo umefanya wagonjwa 78 waliopata huduma hiyo tangu ianze mwaka 2023.

“Huduma hii inafanyika kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani kwa kushirikiana na wataalamu bobezi wa upandikizaji kutoka Korea Kusini wakiongozwa na Daktari bingwa wa upandikizaji Prof Park Kwan Tae wamekuwa wakiwajengea uwezo wataalamu wetu katika eneo hilo”.

DK Delila amesema huduma ya kutengeneza mishipa ya kuchuja damu ina faida nyingi kwa mgonjwa ikiwemo kumpinguzia athari ya kupata maambukizi ya vimelea kama bakteria,inapunguza maudhi madogo madogo na mgonjwa anaweza kuvaa shati la mikono mirefu .

Kuhusu upandikizaji wa figo amesema utaalamu wa kuvuna figo kwa kuputia matundu mpaka sasa hapa nchini unatolewa na Mloganzila pekee.

“Teknolojia hii imekuwa rafiki sana kwa wachangiaji kwani inawafanya wakae wodini kwa muda mfupi sana siku mbili au tatu ,mchangiaji kutokuwa na makovu makubwa yanayotokana na kupasuliwa,”ameeleza Dk Kimambo.

Amesema mpaka sasa wagonjwa 19 wamenufaika na matibabu ya kupandikiza figo tangu huduma hiyo ianze kutolewa mwaka 2023.

“Pamoja na huduma hiyo wataalamu pia walipata fursa ya kubadilishana uzoefu kupitia kongamano la kitaalamu lililohusisha wataalamu 30 kutoka hospitali za hapa nchini na nchi za jirani.

Dk Kimambo ametoa rai kwa jamii kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kula mlo kamili kama inavyoshauriwa na wataalamu pamoja na kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.

“Ikiwemo magonjwa ya moyo,shinikizo la juu la damu na kisukari ambayo yanachangia kuharibu figo ambapo matibabu yake ni gharama kubwa kwa hapa Mloganzila ni takribani Sh milioni 30 na kwa nje ya nchi ni Sh milioni 100,”amebainisha.

Amesema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO)inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya watu duniani wanaugonjwa sugu wa figo na kwa Mloganzila katika kliniki za mara mbili kwa wiki wanaona wagonjwa 20 hadi 30.

“Wagonjwa wanaopata huduma ya kuchuja damu ni zaidi ya wagonjwa 100 ambao wanakuja kupata huduma hii mara tatu kwa wiki,”amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button