UMOJA WA KITAIFA: Somo la milele kutoka kwa Mwalimu Nyerere

DAR-ES-SALAAM : TANZANIA ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimefanikiwa kupata uhuru bila kumwaga damu. Mafanikio haya yanatokana na juhudi na maono ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye aliongoza taifa hili kwa misingi ya umoja na mshikamano.

Mwalimu Nyerere alipambana na changamoto kuu tatu zilizotishia mshikamano wa taifa: ukabila, udini, na ujimbo. Alikuwa na imani kwamba maradhi haya ni hatari kwa utulivu na maendeleo ya taifa, na hivyo alichukua hatua za makusudi kuyakabili. Alionya mara kwa mara kwamba taifa linaloruhusu migawanyiko ya kidini, kikabila, au kiuchumi haliwezi kupiga hatua.

Katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, Mwalimu aliongoza Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961. Baada ya uhuru, alitekeleza sera ya ujamaa na kujitegemea, sera zilizolenga kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuondoa tofauti za kitabaka na kikabila.

Katika moja ya hotuba zake za kihistoria kwenye Mkutano Mkuu wa CCM mwaka 1995, Mwalimu Nyerere alikemea ukabila kwa nguvu zote. Aliwataka Watanzania kuacha kujivunia makabila yao, akisisitiza kuwa jambo hilo halina manufaa kwa taifa. “Kazi ya uongozi ni kujenga watu wawe kitu kimoja, siyo kuwatenganisha,” alisema kwa msisitizo mkubwa.

SOMA: Tanzania ni mfano miaka 63 ya Uhuru

Maneno haya ya Mwalimu bado yana uhalisia hadi leo. Nchi nyingi za Afrika zimejikomboa kutoka kwa ukoloni, lakini bado zinakumbwa na migogoro inayochochewa na ukabila, udini, na maslahi ya kisiasa. Mfano halisi ni Kenya, ambako mivutano ya kikabila imekuwa chanzo cha migogoro ya kisiasa na maandamano yanayoharibu mshikamano wa taifa.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) nayo inakabiliwa na migogoro ya kikabila inayochochewa na masuala ya ardhi, rasilimali, na siasa. Migogoro hii imeendelea kuzorotesha maendeleo ya nchi hiyo, huku juhudi za kimataifa za kuleta suluhisho zikiendelea kukumbana na changamoto kubwa.

Hali hiyo pia imeonekana Sudan na Sudan Kusini, ambako migogoro ya kikabila imesababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Sudan Kusini, kwa mfano, imeshuhudia mapigano makali kati ya makabila makuu ya Dinka na Nuer, hali iliyoleta uharibifu mkubwa na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.

Rwanda ni mfano wa jinsi migogoro ya kikabila ilivyoleta maafa makubwa. Mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambapo Wahutu waliwaua takriban watu 800,000, ni funzo kwa Afrika nzima. Hata hivyo, juhudi za Rwanda kuondoa utambulisho wa kikabila katika nyaraka rasmi zimeleta mafanikio makubwa katika kupunguza mivutano ya kikabila.

Tangu kifo cha Baba wa Taifa mwaka 1999, Tanzania imeanza kushuhudia dalili za ukabila, udini, na ujimbo miongoni mwa baadhi ya wanasiasa. Hali hii ni changamoto kubwa kwa taifa, na inahitaji juhudi za makusudi kutoka kwa viongozi wa sasa ili kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa.

Mwalimu Nyerere alifahamu kwamba ukabila na udini ni hatari kubwa kwa taifa. Alihakikisha kuwa siasa hazitumiwi kama jukwaa la kuendeleza masuala ya kidini au kikabila. Alisimama imara kuhakikisha serikali inabaki kuwa sekula, na kila mtu ana uhuru wa kuabudu bila siasa kuingilia dini.

Leo, baadhi ya wanasiasa wameanza kutumia ukabila na udini kwa manufaa yao ya kisiasa, hali ambayo inatishia amani na mshikamano wa taifa. Kama alivyosisitiza Mwalimu, uongozi wa kweli unapaswa kuunganisha watu, siyo kuwatenganisha.

Watanzania wanapaswa kujifunza kutoka kwa historia ya nchi nyingine za Afrika na kuhakikisha wanadumisha mshikamano, amani, na usalama. Umoja wetu ni silaha kubwa ya kujenga taifa lenye mafanikio.

Tunapomkumbuka Hayati Mwalimu Nyerere, ni muhimu kufuata misingi yake ya haki, mshikamano, na umoja. Hii ndiyo njia pekee ya kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi ya amani na mshikamano kwa vizazi vijavyo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button