TRA makusanyo juu 78% miaka minne

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeongeza makusanyo ya kodi kwa asilimia 78 katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema muda huo makusanyo yameongezeka kutoka Sh trilioni 11.92 mpaka Sh trilioni 21.20.
Mwenda alisema hayo Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya TRA katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Alisema ongezeko la makusanyo hayo ni matokeo ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa TRA.
“Alitoa maagizo matatu makubwa kwa TRA ambayo ni kuhakikisha TRA inakusanya kodi kwa weledi, kupanua wigo wa ukusanyaji kodi na kujenga mahusiano bora na walipakodi, kutumia 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya) na walipakodi,” alisema Mwenda.
Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa katika kutekeleza hayo wameongeza makusanyo ya kodi na ulipaji kodi kwa hiyari na hayo ni sehemu ya mafanikio 10 ya TRA katika miaka minne ya uongozi wa Rais Samia.
“Kwa kipindi cha miezi minane kuanzia Julai 2024 mpaka Februari 2025, TRA imekusanya Sh trilioni 21.20 sawa na ufanisi wa asilimia 104 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 20.42 ambao ni ukuaji wa asilimia 17 ukilinganisha na Sh trilioni 18.06 kilichokusanywa kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliopita, 2023/24,” alisema Mwenda.
Alisema makusanyo hayo ni ongezeko la Sh trilioni 9.28 ambalo ni ukuaji wa asilimia 78 ukilinganisha na Sh trilioni 11.92 kilichokusanywa kati ya Julai 2020 mpaka Februari 2021, kabla Serikali ya Awamu ya Sita haijaingia madarakani.
“Katika miezi minane ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/25, TRA imevuka malengo iliyopangiwa na serikali kwa kila mwezi kwa miezi yote minane mfululizo, mafanikio haya yametokana na utekelezaji wa maelekezo ya Rais aliyoyatoa wakati wa kumuapisha Kamishna Mkuu, Julai mwaka 2024,” alisema Mwenda.
Alisema mafanikio mengine ni kuimarisha uhusiano na wafanyabiashara na wananchi na hapo TRA imekuwa ikishirikiana na wafanyabiashara nchini kujenga uhusiano na kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kibiashara na kikodi za wafanyabiashara.
Alisema walifanya vikao na walipakodi wa ngazi zote wakubwa na wakati kwa kuwafuata walipo katika mikoa yote Tanzania hivyo kuimarisha ushirikiano kati ya TRA na walipakodi.
“Kutenga Alhamisi ya kila wiki kama siku maalumu ya kusikiliza na kutatua changamoto za walipakodi, wito wetu ni kuwaomba walipakodi kutumia siku hii maalumu kukutana na viongozi wa TRA nchi nzima meneja wa tawi, mkoa na makamishna wasaidizi ili kutatua changamoto zao,” alisema Mwenda.
Pia, alisema katika hilo wameimarisha ushirikiano na viongozi wa serikali, viongozi wa dini na makundi mbalimbali na viongozi wa vyama vya michezo, wakiwemo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mwenda alisema mafanikio mengine ni kuwezesha kukua kwa biashara na shughuli za kiuchumi nchini na kuboresha mazingira ya uwekezaji, ikiwemo kurahisisha taratibu za ulipaji kodi na kupunguza urasimu.
Alisema hatua hizo zimevutia wawekezaji na kuongeza wigo wa walipakodi na hivyo kuongeza mapato ya serikali.
“Tumeanzisha mahusiano ya karibu sana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kuwa na timu ya pamoja ya kutatua changamoto za kikodi za wawekezaji na katika miezi minane kati ya Julai, 2020, mpaka Februari, 2021,
marejesho ya kodi yalikuwa ni Sh. milioni 92,372 wakati miakA minne baadae katika kipindi cha Julai, 2024, hadi Februari, marejesho ni Sh trilioni 1.2,” alisema.
Alisema jambo lingine wanalojivunia kwa miaka hii minne ni kuimarisha weledi na uadilifu kwa watumishi wa TRA na katika hilo walichukua hatua kwa watumishi waliokosa weledi kwa mujibu wa sheria.
“Katika kipindi hicho tumefukuza kazi watumishi 14, tulishusha mishahara watumishi sita, tuliwashusha vyeo watumishi 12 na kuwapa onyo la maandishi 22,” alisema.
Akizungumzia mipango ya taasisi hiyo, Mwenda alisema ipo mingi ikiwa ni pamoja na kuajiri watumishi 1,596 kufikia Juni 2025 na kuwatoa hofu Watanzania walioomba nafasi mbalimbali kwamba wenye sifa wataajiriwa.
“Kwa sasa, TRA imejiwekea mikakati mbalimbali ili kuhakikisha kuwa inaendelea kukusanya mapato ya kutosha kwa lengo la kuiwezesha serikali kutekeleza mipango ya maendeleo na kuimarisha huduma za jamii kwa Watanzania,” alisema.
Imeandaliwa na Zena Chande Dar, Magnus Mahenge Dodoma

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button