Asilimia 40 ya wanawake wamefanyiwa ukatili

ASILIMIA 40 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili au kingono mara moja au zaidi katika kipindi cha maisha yao.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt.

Dorothy Gwajima, ameyasema hayo akizungumza na waandishi wa Habari pamoja na wananchi katika soko la Kigogo Fresh, Pugu jijini Dar es Salaam leo Novemba 22, 2022 kuelekea siku 16 za kupinga ukatili.

Dkt. Gwajima amesema taarifa hizo za Utafiti wa Afya ya uzazi na Viashiria vya Malaria inaonesha pia kwa mwaka 2015/16 asilimia 20 ya wanawake wa umri huo wameingiliwa kimwili bila ridhaa yao.

“Katika kupambana na tatizo la Mauaji na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, jamii yote tunatakiwa kuunganisha nguvu kwenye kubuni mikakati ya kijamii ambayo italeta tija na suluhisho la kudumu.

Kwenye maeneo mengi ya nchi kuongezeka kwa uelewa juu ya masuala ya ukatili na madhara yake ni kutokana na utekelezaji wa mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Mwaka 2017/18-2021/22 (MTAKUWWA)” amesema Dkt. Gwajima.

Amebainisha kuwa katika mpango wa MTAKUWWA wa miaka mitano, matokeo chanya yamepatikana kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe na hasa kuwahusisha viongozi wa kijamii wakiwemo viongozi wa dini, viongozi wa kimila, wazee maarufu na watu wengine ambao wana sauti ndani ya jamii.

Ameongeza kwamba, katika kukabiliana na vitendo vya Ukatili wa Kijinsia hapa nchini, Serikali kwa kushirikian na wadau, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili.

Waziri Dkt. Gwajima amewataka wanaume kujitokeza kushiriki kutokomeza vitendo vya ukatili hasa kwa upande wao badala ya kuchukua maamuzi ambayo yana madhara kwa familia na jamii kwa ujumla.

“Serikali kupitia Wizara hii inashughulikia jinsia zote kwa ngazi zote kuanzia Polisi, Magereza, Halmashauri na pia namba 116, elezeni changamoto zenu” ameongeza Waziri Gwajima.

Ameendelea kusema kuwa, kuelekea Siku 16 za Kupinga Ukatili ambapo uzinduzi utafanyika tarehe 25 Novemba, 2022 Serikali kwa pamoja na Wadau itafanya Kampeni katika ngazi zote kuanzia Taifa, Mikoa, Wilaya, Kata na ngazi za Vijiji/Mitaa kulingana na mazingira na taratibu za maeneo husika.

Aidha, amewaasa Wakuu wa Mikoa kutoa Tamko kwa Umma kuhusu uwepo wa Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na Wizara kwa ushirikiano na Wadau wake itafanya ufuatiliaji na kutangaza waliofanya vizuri katika maeneo husika kuhusu mbinu na mikakati ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.

Halikadhalika, Waziri Dkt. Gwajima amesema ngazi zote zinazotekeleza zitaainisha baadhi ya Viongozi wa Serikali, Dini na Kimila, Wataalamu na Watu wenye Ushawishi katika Jamii ambao watakwenda katika vyombo vya habari; luninga na redio hasa redio za kijamii kuzungumzia vitendo vya ukatili wa kijinsia na hasa ukatili dhidi ya watoto katika kipindi chote cha siku 16 za kupinga ukatili.

Akitoa salaam za Shirika linaloshughulika na kupambana ukatili wa kijinsia WILDAF Mkurugenzi wa Shirika hilo Anna Kulaya amesema chimbuko la kampeni hiyo ni mauaji ya kinyama ya wanawake wa Mirabelle yaliyofanyika nchini Domiica mwaka 1960.

Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili mwaka huu inaadhimishwa kwa kaulimbiu isemayo “Kila Uhai Una Thamani: Tokomeza Mauaji na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watotoā€¯ na itazinduliwa Mkoani Dar Es Salaam tarehe 25 Novemba, 2022.

Habari Zifananazo

Back to top button