Tanzania kuunga mkono amani Ukanda wa Maziwa Makuu

CONGO: TANZANIA imeunga mkono ajenda zote muhimu zilizojadiliwa katika Mkutano wa Tisa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR).
Makamu wa Rais, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi alisema hayo wakati akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo uliofanyika Kinshasha nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Alisema Tanzania inaunga mkono ajenda zote muhimu, ikiwemo ya amani na usalama na kusisitiza kuwa itaendelea kutoa mchango mkubwa kama inavyofanya katika nchi mbalimbali kuhakikisha kuwa amani ya kweli inapatikana kwenye kanda hiyo. Mkutano huo ulitanguliwa na vikao vya wataalamu, wakuu wa vyombo vya ulinzi pamoja na Kamati za Mawaziri wa Kisekta, ikiwemo ulinzi, madini na jinsia.
Mkutano huo umebebwa na Kaulimbiu ya “Uimarishaji wa Amani na Usalama kwa Maendeleo Endelevu katika Eneo la Maziwa Makuu.” Kupitia kaulimbiu hiyo, nchi wanachama zimejadili hali ya usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu na kupendekeza njia za kuimarisha amani na usalama kwenye eneo hilo.
Aidha, nchi wanachama zimetakiwa kuenzi mkataba ulioanzisha jumuiya hiyo unaolenga kufikiwa kwa amani, usalama na maendeleo ya kweli kupitia ushirikiano, umoja na mshikamano bila kusahau kujitoa na kujituma kwa hali na mali kufanikisha malengo hayo.
Ajenda zingine zilizojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na masuala ya madini, jinsia pamoja na fedha. Katika hatua nyingine, kwenye ufunguzi wa mkutano huo, Mwenyekiti Mpya wa ICGLR ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi alimpongeza Rais Samia kwa ushindi alioupata katika Uchaguzi Mkuu uliofanywa Oktoba 29, mwaka huu.
Katika mkutano huo, Dk Nchimbi aliambatana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Zanzibar, Salehe Juma Mussa; Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa; Balozi wa Tanzania nchini DRC, Said Juma Mshana pamoja na maofisa waandamizi na wataalamu mbalimbali.



