Ngajilo aahidi Iringa ya michezo, sanaa, ajira 2026

IRINGA: Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo, amefunga mwaka uliopita kwa bonanza lililojaa hamasa, burudani na matumaini mapya kwa vijana wa Iringa, akitumia jukwaa hilo kutangaza dira ya mwaka 2026 inayolenga kuinua michezo, sanaa, na uchumi wa vijana.

Akihutubia mamia ya washiriki wa bonanza hilo lililohusisha michezo ya mpira wa miguu, pete, ngumi, rede, mbio fupi, drafti, kufukuza kuku pamoja, burudani kali kutoka kwa wasanii wa Bongo Fleva na zingine, Ngajilo alisema:

“Hili ni tukio la mshikamano na kuamsha ari ya maendeleo. Tunaanza mwaka mpya tukiwa na dhamira mpya: Kuibua na kukuza vipaji, kujenga miundombinu, na kuweka mazingira rafiki kwa vijana wetu kufanikiwa,” alisema Ngajilo.

Katika hatua iliyopokewa kwa shangwe, Mbunge huyo alitangaza kwamba Manispaa ya Iringa imetenga Sh Milioni 30 kwa ajili ya ukarabati wa Uwanja wa Mlandege, ikiwemo ujenzi wa ukuta na huduma nyingine za msingi.

Alisema uwanja huo utafungua milango kwa matukio makubwa zaidi ya michezo na sanaa katika manispaa hiyo.

Mbali na hilo, Ngajilo aliahidi kuendelea na ugawaji wa vifaa vya michezo kwa timu mbalimbali za mitaani na mashuleni, kuwezesha wasanii kufikia studio bora na kupata mafunzo ya sanaa, kuanzisha programu za ujasiriamali kwa vijana, na kufanya bonanza kuwa tukio la mara kwa mara kila mwaka ili kuibua vipaji.

“Iringa inatakiwa kutoa akina Diamond Platnumz wengine, Samatta wengine… vijana wenye vipaji wasibaki nyuma kwa sababu ya ukosefu wa fursa. Sisi kazi yetu ni kuwafungulia njia,” alisisitiza.

Ngajilo aliwaasa vijana kudumisha nidhamu na mshikamano, akisema maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana pasipo ushirikiano wa pamoja.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button