TRA yavunja rekodi, yakusanya tril 9.8/-

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imejivunia ufanisi wa ukusanyaji wa mapato katika robo ya pili ya Mwaka 2025/2026 huku Desemba ikivunja rekodi za ukusanyaji wa mapato nchini kwa kukusanya Sh trilioni 4.13 sawa na asilimia 102.9.

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akitoa salamu za Mwaka Mpya wa 2026 na taarifa ya utendaji katika kipindi cha nusu ya kwanza ya Mwaka 2025/2026. Amesema ili kuwa na mwendelezo mzuri wa ulipaji kodi, TRA imeanzisha mfumo wa ulipaji kodi utakaoanza kufanya kazi mwezi huu ambapo kodi zote zitalipwa kimtandao hali itakayosaidia kuondoa malalamiko yakiwemo ya ukadiriaji usioendana na uhalisia pamoja na rushwa.

Amesema katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, TRA imekusanya Sh trilioni 9.8, sawa na ufanisi wa asilimia 101.45 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 9.66. Makusanyo haya ni sawa na ukuaji wa asilimia 12.26 toka Sh trilioni 8.73 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2024/2025. SOMA: Tume ya Madini, TRA kuongeza ufanisi ukusanyaji maduhuli

Aidha, ameeleza kuwa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 kinachoanza Julai hadi Desemba 2025, TRA imefanikiwa kukusanya Sh trilioni 18.77 sawa na ufanisi wa asilimia 103.7 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 18.10. Amesema makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 13.6 ikilinganishwa na Sh trilioni 16.52 kilichokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2024/2025.

Kwa upande wa makusanyo ya Desemba, 2025 ambayo ni Sh trilioni 4.13, ni ya juu kabisa kukusanywa na TRA ndani ya mwezi mmoja toka mamlaka ilipoanza shughuli zake na kuvunja rekodi ya kile kiwango cha juu kilichowahi kukusanywa mwezi kama huo mwaka 2024 ambacho ni Sh trilioni 3.58.

“TRA imeweza kurekodi ukuaji chanya wa asilimia 13.6 katika kipindi cha Julai hdi Desemba 2025, hali inayoonesha matokeo chanya ya bidii za mamlaka kusimamia mapato ya serikali pamoja na juhudi za serikali kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini,” aliongeza Mwenda.

Amesema makusanyo yaliyokusanywa kwenye nusu ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 ni sawa na ukuaji wa asilimia 103.1 ikilinganishwa na Sh trilioni 9.24 kilichokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2020/2021.

Kwa mujibu wa Mwenda, sababu zilizochangia ufanisi wa juu katika makusanyo ni ushirikiano mzuri kati ya TRA na wafanyabiashara pamoja na viongozi wa vyama vya wafanyabiashara wote nchini. Pia, uhusiano mzuri kati ya TRA na wadau wake yalisababisha walipakodi wote kushiriki kikamilifu kukamilisha matakwa yao ya kisheria ya kulipa kodi

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button