Mauzo korosho yavuka tril 1.2/-

MAUZO ya korosho kwenye minada mbalimbali nchini yamevunja rekodi baada ya kuvuka Sh trilioni 1.2 ambazo zimekusanywa nchini, kutokana na kuuzwa tani 433,000 za korosho msimu huu unaotarajiwa kukamilika Machi 2026.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho nchini, Francis Alfred amesema hayo mkoani Mtwara na kuzitaja takwimu hizo kuwa bora, ikilinganishwa na misimu iliyopita ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kumekuwepo na ongezeko la jumla la mauzo ya korosho.

Alfred amesema mauzo ya korosho kwenye minada nchini yamepanda kutoka tani 271,000 mwaka 2023/2024 na kupaa hadi 409,000 kwenye minada ya mwaka 2024/2025 na sasa hivi msimu huu wa mwaka 2025/2026 ambao unaendelea, mauzo yamepaa hadi kufika tani 433,000. “Minada bado inaendelea, hususan katika mikoa ya Kanda ya Kati pamoja na mikoa mingine ambayo bado inaendelea kuuza korosho kwenye minada,” alieleza Alfred.

Amesema mafanikio hayo yanatokana na maboresho yaliyofanywa kwenye mnyororo mzima wa thamani wa zao la korosho. “Wakulima sasa hivi wanaweza kudhibiti magonjwa na wadudu kwenye mazao bila changamoto yoyote, kwa sababu kila mkulima aliyesajiliwa anapewa pembejeo za ruzuku bila shida yoyote.

Pia, kumekuwa na maboresho makubwa kwenye huduma za ugani,” alisema. Amesema changamoto za uhifadhi wa korosho zimechangia kwa kiwango fulani kupungua kwa kiwango cha mauzo kwa Chama Kikuu cha Ushirika (MAMCU). Meneja wa MAMCU, Blandina Matipa alisema hadi sasa wameuza tani 114,000 ikiwa ni pungufu ya tani 4,000, ikilinganishwa na msimu uliopita.

Wakulima wa korosho katika mikoa ya Kusini wanatamani kuona bei ya korosho ikipanda angalau kuuzwa kwa Sh 4,000 kwa kilo moja, tofauti na Sh 2,500 ya sasa ili kumfanya mkulima apate faida kulingana na jasho analomwaga shambani. SOMA: MAMCU yaingiza bil 207/- mauzo ya korosho

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button