Bodi ya Ithibati yaonya waandishi wasio na sifa

DAR ES SALAAM; Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imesema imebaini baadhi ya watu wasio na sifa wamerejea kutekeleza majukumu ya kihabari baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu.
Taarifa iliyotokewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Patrick Kipangula leo Januari 7, 2026, imesisitiza kuwa uandishi wa habari ni taaluma rasmi inayosimamiwa kwa misingi ya kisheria, maadili na weledi wa kitaaluma na hivyo mtu yeyote anayejihusisha na shughuli za kihabari bila kuwa na ithibati anakiuka masharti ya Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229(Toleo la 2023).

“Aidha, kwa mujibu wa Kanuni ya 17(1)(a) ya Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari, Tangazo la Serikali Na. 18 la Tarehe 3 Februari, 2017 wanaopaswa kuwa na ithibati ni pamoja na wahariri, waandishi wa habari, waandishi huru (freelancers), wapiga picha, wazalishaji wa vipindi na watangazaji wa redio na televisheni wanaofanya kazi katika vyombo vya habari.
“Kwa muktadha huo, Bodi inatoa onyo na kuwataka watu wote wanaofanya kazi za kihabari bila kuwa na ithibati kuacha mara moja, kwani kuendelea kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa Kifungu cha 50 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.

“Aidha, Bodi haitasita kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya mtu au taasisi yoyote itakayobainika kuajiri au kuruhusu utekelezaji wa shughuli za kihabari bila kuzingatia utaratibu na masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa Sheria.
“Vilevile, Bodi inautaarifu umma na wadau wote wa sekta ya habari kuwa katika kipindi cha hivi karibuni itaendesha ukaguzi maalum katika vyombo vya habari na maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kujiridhisha kuwa watu wote wanaotekeleza majukumu ya kihabari wanakidhi vigezo vilivyoainishwa kwa mujibu wa Sheria.
“Ikumbukwe kuwa, utoaji wa ithibati kwa waandishi wa habari si kikwazo cha uhuru wa habari, bali ni nyenzo muhimu ya kulinda heshima na hadhi ya taaluma ya uandishi wa habari, kuongeza uaminifu wa taarifa zinazozalishwa na kusambazwa kwa umma, pamoja na kuwapatia waandishi ulinzi wa kisheria wanapotekeleza majukumu yao,” imesema taarifa hiyo.
Bodi inatoa wito kwa watu wote wenye nia ya kufanya kazi za kihabari kuhakikisha kuwa wanapata ithibati kwa mujibu wa sheria, wanazingatia maadili na weledi wa juu wa taaluma, na kutumia kalamu, sauti na majukwaa yao kwa kuwahudumia wananchi kwa kutoa taarifa sahihi, kukuza uwajibikaji, na kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.



