Dk Mwinyi aanika mafanikio lukuki afya, amani, Muungano

ZANZIBAR; WAKATI Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar leo ikiadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais Dk Hussen Mwinyi amesema serikali yake inajivunia mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Akitoa Hotuba ya Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi jana, Dk Mwinyi alisema miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka 62 ya Mapinduzi ni kuimarisha amani na utulivu.

Muungano waimarika

Alisema Mapinduzi ya Zanzibar yamefanikisha kuimarisha Muungano wa Tanzania kisiasa, kiuchumi na kijamii.

“Serikali zetu mbili zimeendeleza utaratibu wa kushughulikia hoja za Muungano kwa pamoja. Kwa kipindi cha karibuni, jumla ya hoja 15 za Muungano zimejadiliwa na kuondoshwa na hati 13 za maamuzi zimesainiwa,” aliongeza Dk Mwinyi.

Ukuaji wa uchumi

Aidha, alisema katika miaka 62 ya Mapinduzi Wazanzibari wanajivunia mafanikio katika ukuaji wa uchumi kutokana na juhudi walizozifanya katika usimamizi wa sera za uchumi na fedha pamoja na makusanyo ya mapato kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki na upatikanaji wa mitaji, zimewezesha kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Alifafanua kuwa kutokana na hayo, uchumi wa Zanzibar umeendelea kuimarika vyema ambapo kwa mwaka 2024, umekua kwa kasi ya asilimia 7.1 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 1.3 mwaka 2020.

Kadhalika, pato la taifa kwa bei ya soko limeongezeka kufikia Sh trilioni 6.57 kwa mwaka wa 2024 kutoka Sh trilioni 4.78 mwaka 2021.

Pia, ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka Sh bilioni 856 mwaka 2020/2021 hadi kufikia Sh trilioni 2.104 mwaka 2024 na kwamba serikali imefanikiwa kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kubaki katika tarakimu moja hadi kufikia asilimia 5.

Aliongeza kuwa kufikia mwisho wa Desemba 2025, uwekezaji ulifika jumla ya miradi 1,657 yenye mtaji wa Dola za Marekani bilioni 20.206 ilisajiliwa na Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).

Sekta ya utalii

Dk Mwinyi alieleza mipango ya kuimarisha sekta ya utalii na kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Zanzibar kwa kuendeleza utalii wa matamasha ya michezo na utamaduni, makongamano na mikutano ya kimataifa pamoja na kuendeleza urithi wa majengo ya kale. 

Ajira kwa vijana

Katika kukabiliana na changamoto za ajira hasa kwa vijana, Dk Mwinyi alisema serikali inaendelea kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia vikundi vipya 1,293 vilivyoanzishwa na klabu za vijana zenye wanachama 3,799.

“Serikali imetoa fursa za ajira mpya 742 kati ya Januari na Desemba, 2025 kwa kada maalumu ili kuongeza nguvukazi na kuziba mapengo ya wastaafu katika kuongeza rasilimaliwatu katika sekta ya umma,” alisema.

Aliongeza kuwa jumla ya miradi 37 ya vijana ya Sh bilioni 28.9 imetekelezwa kwa ushirikiano wa serikali na wadau wa maendeleo ikihusisha ubunifu wa kidijiti, kilimo, lishe, stadi za maisha na ujasiriamali.

“Katika kipindi hiki, serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na uzalishaji kwa vijana 500 na kuwaunganisha na fursa za masoko kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi,” aliongeza Dk Mwinyi.

Mapambano dhidi ya rushwa

Kwa upande wa rushwa, alisema serikali kupitia Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kati ya Januari hadi Desemba 2025, imefanikiwa kuokoa Sh bilioni 6.687 na Dola za Marekani 94,370.

Utumishi waimarishwa

Alisema serikali imeimarisha matumizi ya miundo ya utumishi ambapo hivi sasa inatumika kwa ufanisi katika kupandisha vyeo, madaraja na marekebisho ya mishahara kuanzia mwaka 2022 jambo ambalo limewezesha kuondoa malalamiko.

Rais Dk Mwinyi alisema serikali itatoa mikataba ya utumishi na kuweka mifumo maalumu ya usimamizi wa nidhamu na utendaji wa watumishi wa umma ili kuondokana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na kutozingatia kanuni na sheria za utumishi.

Aidha, kupitia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, kwa ushirikiano na serikali, wananchi 422,908 kutoka mikoa na wilaya zote Zanzibar walipata huduma za kisheria wakiwemo wanawake 209,185 na wanaume 213,723.

Hadi kufikia Desemba 2025, jumla ya diaspora 1,283 wamesajiliwa katika kanzidata.

“Kwa mujibu wa usajili uliofanyika kuna wawekezaji wakubwa na wadogo 55 waliowekeza miradi hapa Zanzibar ikiwemo ya afya, elimu, ujenzi wa hoteli na miradi mingine ya uchumi,” alisema.

Alisema kupitia Mfumo wa Sema na Rais (SNR), malalamiko 21,725 yamepokelewa kutoka kwa wananchi ambapo malalamiko 19,008, sawa na asilimia 87.5 tayari yamepatiwa ufumbuzi. Malalamiko 2,717, sawa na asilimia 12.5 yanaendelea kushughulikiwa.

 Mafanikio vita dhidi ya umaskini

Dk Mwinyi alisema kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa mwaka 2025, miradi 23 ikiwemo 16 ya elimu na saba ya afya inayohusisha ujenzi wa miundombinu imetekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 4.655.

Alisema Sh bilioni 56.107 zimetolewa ili kuzisaidia kaya masikini hapa Zanzibar. Hadi Septemba 2025, huduma zinazotolewa kupitia Mpango wa kunusuru kaya maskini wa Tasaf awamu ya tatu (TASAF III) zimewafikia walengwa wa shehia zote 388 za Zanzibar na kuzinufaisha kaya 53,636.

 

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button