Wadau wampongeza Dk Mwinyi kuwaunganisha Wazanzibari
WADAU wa uchumi na siasa wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ally Mwinyi kwa kutekeleza dhana ya Mapinduzi kwa vitendo Zanzibar.
Wakizungumza na gazeti la HabariLEO, walisema Dk Mwinyi amefanikiwa kuwaunganisha Wazanzibari na kuwafanya kuwa kitu kimoja kwa kuweka uwiano mzuri wa kimaendeleo katika Visiwa vya Unguja na Pemba.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib alisema kitendo cha Dk Mwinyi kuanzisha na kukamilisha miradi mingi Pemba kimewafanya wananchi kuona fahari na kujihisi ni sehemu ya Zanzibar.
Alisema chini ya Dk Mwinyi, vijana wote wa Kizanzibari bila kubagua mahali anapotoka wanapata fursa sawa za ajira serikalini tofauti na kipindi cha nyuma ambapo hakukuwa na fursa sawa kwa vijana.
“Sasa hivi katika soko la ajira, hakuna tena kuangalia mahali anapotoka kijana ili mradi ni Mzanzibari kutoka Pemba au Unguja wote wana haki sawa katika serikali ya Dk Hussen Mwinyi,” aliongeza Khatib.
Aidha, alisema miaka 62 ya Mapinduzi imeimarisha Muungano kwa sababu bila ya mapinduzi hayo hata Muungano usingekuwepo.
Kwa upande wake Mwanasiasa mkongwe, Paul Kimiti ambaye alikuwepo wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar, alisema kutokana na misingi mibaya ya ubaguzi iliyoachwa na wakoloni baada ya mapinduzi, Rais Abeid Amani Karume aliamua kuruhusu Waswahili kuoa na kuolewa na Waarabu.
Alisema lengo la Karume kuruhusu ndoa hizo ni kuvunja ukuta wa kibaguzi uliowekwa na wakoloni, kuwafanya Waswahili waliodharauliwa na kubaguliwa kutokana na rangi ya ngozi zao, kurudisha hadhi ya wananchi waliokata tamaa kutokana na kudharauliwa katika jamii.
“Wakaanza kuzaliwa watoto chotara ambao waliua kabisa ule ufalme wa waarabu kwa kuwa watawezaje kuwadharau Waswahili wakati wameungana na kuunda familia,” alisema Kimiti.
Alieleza kuwa kwa kuunda familia moja na kuchanganya damu za Waswahili na za Kiarabu, Waswahili walianza kujiamini na kujiona ni kitu kimoja na kwamba ni sehemu ya Wazanzibari wenye haki sawasawa na wengine ambao hapo awali walionekana bora kuliko wengine.
Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Gabriel Mwang’onda alisema baada ya Mapinduzi viongozi walioiongoza Zanzibar walikuwa na kibarua kipevu cha kuhakikisha kuwa hali hiyo wanaiondoa na kujenga maisha ya Wazanzibari.
“Lakini pili wananchi wanaona umuhimu wa kujitawala wenyewe baada ya kubaguliwa kwa miaka nenda rudi hatimaye wanaanza kunufaika na rasilimali walizojaliwa na Mwenyezi Mungu,” alisema Mwang’onda.
Wakati huohuo, mdahalo wa wazi uliofanyika jana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ulioandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa chuo hicho (UDASA) umeibua mawazo mseto kuhusu mchango wa Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha maisha ya Watanzania kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Akichangia mada kuu ya mdahalo huo inayosema ‘Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 yalikuwa muhimu na lazima’, Makamu wa Rais wa Umoja wa Wanafunzi wa chuo hicho (DA- RUSO), Joyce Semkuyu alisema vijana wanapaswa kutumia maarifa na bunifu zao kutekeleza malengo ya Mapinduzi.
Joyce ambaye alichangia mada inayosema ‘Mchango wa vijana (Gen Z) katika kulinda na kudumisha Mapinduzi’, aliwataka Watanzania hasa vijana kuyatafsiri malengo ya Mapinduzi kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuondoa umasikini.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Siasa, Uenezi na Mafunzo, Ally Bananga alisema chama hicho kina jukumu la kudumisha mioyo ya kimapinduzi baina ya wanachama na Watanzania kwa ujumla.
Alisema CCM inalinda na kuuenzi Muungano ambao ndio zao la Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kudumisha amani na utulivu na kutoa elimu kuhusu faida za Muungano kwa Watanzania.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR – Mageuzi, Martin Mung’ong’o alisema vyama vya upinzani vina wajibu wa kutekeleza Mapinduzi kwa kuimarisha demokrasia ya ndani na nje ya chama.
“Vyama vya upinzani vinapaswa kuenzi Mapinduzi kwa ku-hakikisha katiba ya nchi inafuatwa na Watanzania pamoja na chama tawala, vina wajibu wa kuimarisha amani na utulivu pamoja na kuchagiza chaguzi huru na haki,”alisema Mung’ong’o.
Akieleza mchango wa wanataaluma na wanazuoni katika kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Sabatho Nyamsenda alisema UDSM imekuwa ikitekeleza jukumu lake kama chemchemi ya mijadala ya kitaifa.
Alisema wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alifika mara kwa mara kuungana na wanafunzi kujadili masuala ya taifa, hivyo viongozi watekeleze wajibu kama Mapinduzi.



