Mwigulu azuia kutatua kero kwa barua

SERIKALI imeagiza taasisi za serikali ziache kutatua kero za wananchi kwa kuandikiana barua. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza wahusika kwenye taasisi hizo waonane ana kwa ana kwa sababu ofisi za serikali zipo pamoja katika Mji wa Kiserikali wa Mtumba mkoani Dodoma.
Akikagua na kutembelea majengo ya serikali yaliyokamilika na kuanza kutumika likiwamo la Wizara ya Maji. Dk Mwigulu amesema utaratibu wa taasisi za serikali kuandikiana barua unachelewesha utatuzi wa kero na huduma kwa wananchi.
Amesema hakuna mantiki ya kuandikiana barua wakati watendaji wanaweza kukutana ana kwa ana na kutatua changamoto kwa haraka. “Unaandikaje barua wakati ofisi zinaangaliana? Mkutane kwa miguu, tatueni kero za wananchi. Kuandika barua na kusubiri majibu kunachelewesha maamuzi, hatuhitaji kuandikiana barua,” alisema Dk Mwigulu.
Amesema endapo kuna haja ya kuwa na kumbukumbu za kiofisi kwa taarifa za kiserikali, wahusika wanapaswa kuandika muhtasari wa kikao baada ya kukutana, badala ya kuendeleza mlolongo wa barua unaochukua muda mrefu. “Haya ni maelekezo kwa ofisi zote za serikali baada ya kuhamia hapa Mtumba tumieni njia hii kutatua kero za Watanzania, hatuna kisingizio tena, majengo yako tayari na yako jirani, tutatue matatizo kwa kuonana ana kwa ana,” alisisitiza Dk Mwigulu.
Ameongeza: “Nimekuwa nikiona kwenye vikao taarifa ya utekelezaji inasema barua imeshaandikwa, mnaandikaje barua ofisi zinatazamana? Tukwamue hilo barua ikiandikwa majibu wakati mwingine ni hadi mwezi mmoja, hili la barua linachelewesha”. SOMA: Mwigulu aelekeza imani itafsiri uadilifu, uwajibikaji, bidii ya kazi
Aidha, Dk Mwigulu amewataka wakuu wa taasisi kuwawajibisha watumishi wanaoendelea kutumia mfumo wa barua kufuatilia masuala yanayohitaji ufumbuzi wa haraka, akisisitiza kuwa tabia hiyo izingatiwe katika tathmini ya utendaji kazi na wahusika wapunguziwe alama. Akizungumzia kuhamia kwa Makao Makuu ya Serikali mkoani Dodoma, Waziri Mkuu alisema serikali imeingia gharama kubwa za upangaji wa ofisi baada ya uamuzi wa kuhamishia Makao Makuu Dodoma.
Hivyo ujenzi sasa umekamilika na taasisi zote za serikali watambue Makao Makuu ya nchi ni Dodoma na kazi na wahamie hapo. “Nizielekeze taasisi zote za serikali kuwa makao makuu ni Dodoma, hapa Dodoma tumehamia na si kambi ni makao makuu, hatutakuwa na makao makuu mengine au kuwa na ofisi sambamba,” alisema Dk Mwigulu.
Aidha, amezionya taasisi ambazo zimekamilisha ujenzi katika mji huo na hawajahamia na wana ofisi nyingine nje ya hapo au taasisi za serikali zinazopanga badala ya kuhamia mji huo, kuwa jambo hilo si sawa. “Waziri (Lukuvi) mwelekeze Katibu Mkuu (wa wizara hiyo), atengeneze timu ifanye tathmini ya majengo yote ya serikali yaliyoko Dar es Salaam ‘underutilized’ (yanayotumika kidogo) ili niyagawe kwenye taasisi nyingine ambazo zinapanga wakati serikali ina majengo mengine yasiyotumika,” aliagiza.
Amesema wanataka kuona kazi za serikali zinafanywa ndani ya Makao Makuu ya nchi ili kusogeza huduma kwa Watanzania karibu kipa upande. “Makao Makuu ya nchi ni Dodoma. Hapa si kambi, ni makao makuu. Hatutakuwa na ofisi sambamba,” alisisitiza Dk Mwigulu. Katika ziara hiyo, aliipongeza Wizara ya Maji kwa kukamilisha ujenzi wa jengo lake jipya katika Mji wa Kiserikali wa Mtumba, akilitaja kuwa la viwango vya kimataifa na lenye mazingira yanayowezesha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa sita uliogharimu Sh bilioni 22.9 umekamilika, na lina uwezo wa kuchukua watumishi 518. Alisema wizara hiyo haina tena kisingizio cha kutotekeleza majukumu yake kwa weledi.
“Hatuna kisingizio tena, tutafanya kazi. Tuna jengo zuri na tunamshukuru Rais Samia kwa kutuwezesha kulikamilisha,” alisema Aweso. Awali, akizungumzia ujenzi wa majengo ya ofisi za serikali katika mji huo wa kiserikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na wenye Ulemavu), William Lukuvi amesema jumla ya majengo 29 yamejengwa yakiwamo 24 ya wizara mbalimbali na matano ya taasisi za serikali. “Tunamshukuru Rais Samia kwa sababu majengo haya yamejengwa awamu ya pili ya ujenzi wa majengo katika Awamu ya Sita ya uongozi wa Rais Samia,” alisema Lukuvi.



