Mwigulu aelekeza imani itafsiri uadilifu, uwajibikaji, bidii ya kazi

WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ametaka imani ya dini wanayojifunza na kuimarishwa katika ibada itafsiriwe kwa matendo ya uadilifu, uwajibikaji na bidii katika kazi. Amesema lengo ni kujenga taifa lenye hofu ya Mungu na liwe kwenye matendo ya kuheshimu sheria na kushiriki katika kujenga taifa lenye haki, amani na maendeleo endelevu.
Dk Mwigulu ameeleza hayo aliposhiriki Ibada ya Jumapili katika Kanisa Kuu Anglikana la Roho Mtakatifu Dodoma. “Imani ya kweli inapaswa kuonekana kwa matendo,” alisisitiza. Amesema serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini kujenga taifa lenye hofu ya Mungu, upendo, haki na uwajibikaji.
“Sote tunatambua kwamba taasisi za dini zina nafasi ya kipekee ya kuhubiri na kufundisha maadili ya upendo, uvumilivu na kuheshimiana, ambazo ni nguzo kuu za amani ya taifa na Rais Samia Suluhu Hassan anatambua na kuthamini sana mchango mkubwa wa taasisi za dini ikiwemo Kanisa la Anglikana, katika kudumisha amani, maadili mema na mshikamano wa kitaifa,” alisema.
Amesema ibada za Jumapili ni sehemu muhimu ya maisha ya Mkristo na ni muda wa kujitathmini, kuimarisha uhusiano wao na Mungu, na kujifunza namna bora ya kuishi kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu katika familia, jamii na taifa kwa ujumla. SOMA: Rais Samia: Amani ndio nguzo ya uwekezaji
Amesema Watanzania wanakumbushwa kuishi kwa misingi ya upendo, unyenyekevu, haki na uwajibikaji. Dk Mwigulu alisema Tanzania imeendelea kuwa kielelezo cha amani, umoja na mshikamano katika ukanda wetu na barani Afrika. “Amani hii si jambo la bahati, bali ni matokeo ya jitihada za pamoja za serikali, taasisi za dini, familia na wananchi kwa ujumla,” alisema.
Kadhalika, ametoa wito kwa waumini wote na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuwa mabalozi wa amani katika familia zao, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla kupinga vitendo vyovyote vya chuki, migawanyiko na vurugu.
Awali, Askofu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk Dickson Chilongani ameipongeza serikali kwa kuendelea kushirikiana na taasisi za kidini likiwemo Kanisa Anglikana na kwamba wapo pamoja na nayo katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani. “Tunataka nchi iwe na amani ili shughuli ziendelee na hatutachezea amani,” alisema.


