‘Zaka nyenzo muhimu kupambana na umasikini’

DAR ES SALAAM: IMEELEZWA kuwa mfumo wa utoaji zaka katika dini ya Kiislamu ni nyenzo muhimu katika kupambana na umaskini, hususan miongoni mwa wajane.

Hayo yameelezwa katika hafla ya ugawaji wa zaka kiasi cha Sh milioni 50 kwa watu 100 iliyotolewa na Taasisi ya Baitulmaal Tanzania katika Msikiti wa Kisumu, Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam, ambapo wanawake wajane wamejitokeza kuwa wanufaika.

Katika mgawanyo huo, wajane walipewa kipaumbele kutokana na mahitaji yao makubwa ya kiuchumi na kijamii, hususan jukumu la kulea familia bila msaada wa wenza wao.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu wa Bodi na Mtendaji Mkuu wa Baytulmaal, Rubibi, alisema kuwa uwezeshaji wa wajane una athari chanya kwa familia na jamii kwa ujumla.

“Ukimsaidia mama, unasaidia familia nzima. Kwa wajane, unakuwa umewasaidia watoto wao pia ambao wengi wao ni yatima,” alisema.

Alieleza kuwa pamoja na wajane, mgao huo pia uliwahusisha wanafunzi wenye changamoto za kielimu, wajasiriamali wadogo waliokumbwa na majanga, pamoja na watu wenye madeni makundi ambayo yanatajwa miongoni mwa walengwa wa zaka kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa viongozi wa taasisi hiyo, utoaji wa zaka una dhima pana zaidi ya ibada, ukiwa ni mfumo wa kijamii na kiuchumi unaolenga kupunguza umaskini kwa kasi kwa kusambaza rasilimali kutoka kwa wenye nacho kwenda kwa wasio nacho.

Mwenyekiti wa Baytulmaal Tanzania, Sheikh Dk Ibrahim Ghulam, alisema mfumo huo unasaidia kupunguza pengo la kipato katika jamii.

“Yule mwenye ziada akifikia kiwango fulani anatakiwa kutoa sehemu ndogo ya mali yake ili kusaidia wasio na uwezo wa kupata mahitaji yao ya lazima… katika mambo yanayoweza kupunguza umaskini kwa kasi kubwa sana ni utoaji wa zaka,” alisema.

Baadhi ya wanufaika walieleza jinsi msaada huo ulivyobadili maisha yao. Ashura, mfanyabiashara mdogo aliyepoteza mali zake baada ya soko la Ubungo Mawasiliano kuungua, alisema msaada huo umemrejeshea matumaini ya kujitegemea.

“Nilikuwa nimepoteza mwelekeo kabisa, lakini sasa ninaweza kuanza upya biashara yangu,” alisema.

Ukiacha wajane, sehemu ya fedha hizo za zakailielekezwa kwa wafanyabiashara waliopoteza mali zao kufuatia moto ulioteketeza vibanda katika soko la Ubungo Mawasiliano, tukio lililosababisha wengi kupoteza mitaji na bidhaa zao.

Aidha, familia zilizoathirika na mvua kubwa katika kijiji cha Doda, wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, zilijumuishwa miongoni mwa walengwa, baada ya mafuriko kuharibu makazi na shughuli zao za kiuchumi.

Rubibi, alisema msaada huo haukulenga tu kutoa nafuu ya muda mfupi, bali pia kuwasaidia walengwa kurejea katika shughuli zao za uzalishaji. “Lengo letu si kuwasaidia kwa muda mfupi tu, bali kuwajengea uwezo wa kusimama tena kiuchumi. Kwa wafanyabiashara waliopoteza kila kitu, huu ni mwanzo wa kurejea kwenye biashara zao,” alisema.

Mmoja wa wanufaika, Ashura Haruna, mfanyabiashara mdogo aliyeathirika na moto wa Ubungo, alisema tukio hilo lilimuacha bila mwelekeo. Baada ya soko kuungua, nilihisi nimepoteza kila kitu. Lakini msaada huu wa zaka unanipa nafasi ya kuanza upya,” alisema.

Baytulmaal ni taasisi ya kitaifa inayoendeshwa kwa ushirikiano wa taasisi mbili kubwa za Kiislamu Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay’atul Ulamaa) na Umoja wa Wataalamu wa Kiislamu Tanzania (TAMPRO) ikiwa na lengo la kuwawezesha Waislamu kutekeleza ibada ya kutoa zaka ambayo ni nguzo ya tatu ya Uislamu.

Taasisi hiyo hufanya kazi kama daraja kati ya watoaji wa zaka na wanufaika, ili kuhakikisha misaada hiyo inawafikia wanaostahili.

Katika hafla hiyo, viongozi pia walisisitiza umuhimu wa Waislamu wenye uwezo kutekeleza wajibu wa kutoa zaka, wakieleza kuwa kitendo hicho si hisani bali ni haki ya walengwa.

Naye Juma Nchia, aliyepokea msaada kwa niaba ya taasisi inayolea yatima, alionya kuwa kushindwa kutoa zaka kwa wale wanaostahili kufanya hivyo ni kuwanyima haki watu wanaohitaji msaada huo.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. I quit working at shoprite and now I make $65-85 per/h. How? I’m working online! My work didn’t exactly make me happy so I decided to take a chance on something new… after 4 years it was so hard to quit my day job but now I couldn’t be happier.
    .
    You can check more.=== http://www.giftpay7.vip

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button