Serikali yachukua hatua za kiusalama mgodi wa Msasa-Geita
SERIKALI imeweka wazi kuwa tayari imechukua hatua madhubuti kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika mgodi wa Msasa-Runzewe wilayani Bukombe na kumaliza taharuki iliyojitokeza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Safia Jongo amesema hayo baada ya kusambaa kwa taarifa zinazodai uwepo wa vurugu katika eneo hilo.

Kamanda Jongo kupitia taarifa yake kwa umma ametaja hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuzima jaribio la vurugu mgodini hapo kutoka kwa baadhi ya wachimbaji.
Amesema vurugu hizo ziliripotiwa Januari 22, 2026 saa 3 asubuhi katika eneo la Msasa kata ya Runzewe zilizochochewa na wachimbaji wadogo wanaokadiriwa kuwa 1,000.
Kamanda Jongo amesema vurugu zilifuatia zuio kwa wachimbaji wadogo kuendelea na shughuli zao kwenye baadhi ya maeneo kutokana na hali ya usalama kuwa mbaya ikiwemo baadhi ya maduara kujaa maji.
Amesema mazingira hayo hatarishi yalisababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha sambamba na baadhi ya maduara kuwa na milipuko ambayo haikukamilika kulipuka.
“Baada ya katazo wachimbaji wadogo walianzisha vurugu na kurusha mawe kwa nia ya kuwadhuru wasimamizi wa mgodi huo sambamba na kufunga barabara kuu ya Bukombe.
“Kufuatia vurugu hizo jeshi la polisi lililazimika kuwatawanya watuhumiwa kwa mujibu wa sheria na kufanikiwa kurejesha hali ya utulivu na usalama katika mgodi huo”, ameeleza.
Amesema baada ya kuzimwa kwa vurugu hizo wananchi waliruhusiwa kuendelea na shughuli zao kama kawaida ikiwemo uchimbaji na hakuna mtu aliyeshikiliwa ama kukamatwa.
“Hata hivyo mamlaka za serikali zimelazimika kuyafunga maduara 33 kati ya hayo, maduara 17 yalikuwa ndani ya hifadhi ya barabara huku mengine 16 yalikuwa na hali mbaya ya usalama”.
Awali Mkuu wa wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Pasikasi Mulagiri alikanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai wachimbaji wadogo wamefukuzwa eneo hilo.
Amesema hatua zote zilizochukuliwa zililenga kuhakikisha mazingira bora ya kazi kwa wananchi wote pasipo kuathiri usalama wao pamoja na kushughulikia malalamiko yaliyokuwepo.



