Prof. Mkumbo rasmi kusaka wawekezaji Uingereza

LONDON: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amewasili jijini London kuanza ziara rasmi ya kikazi nchini Uingereza iliyoanza Januari 22 hadi 27, 2026, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza.
Baada ya kuwasili, Prof. Mkumbo alifanya kikao cha kazi katika Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini London, ambapo alikutana na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mbelwa Kairuki. Katika kikao hicho, walijadili masuala mbalimbali yanayohusu kuimarisha mahusiano ya kiuchumi, kuboresha mazingira ya uwekezaji pamoja na fursa zilizopo kwa wawekezaji wa Uingereza nchini Tanzania.
Ziara hiyo inaashiria mwanzo wa utekelezaji wa ratiba ya mikutano na shughuli mbalimbali, ikiwemo kukutana na wawekezaji, taasisi za kifedha, makampuni ya kimataifa pamoja na wadau wa maendeleo. Lengo kuu ni kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania na kuendeleza diplomasia ya uchumi.

Katika ziara hiyo, Prof. Mkumbo anaambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kutumia diplomasia ya uchumi kama nyenzo muhimu ya kuvutia uwekezaji, kukuza uchumi wa taifa na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi.




