Waalikwa kuwekeza kiwanda cha Kahawa Nyasa

DODOMA; WIZARA ya Viwanda na Biashara imewaita wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika kiwanda cha kukoboa kahawa kilichopo Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, leo Februari 2, bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Nyasa, John Nchimbi.

Katika swali lake, Mbunge huyo ametaka kufahamu mpango wa Serikali wa kujenga kiwanda cha kukoboa kahawa cha Nyasa, kama ilivyoahidiwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Katika majibu yake Waziri Londo amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa huzalisha kahawa aina ya Arabica kwa wastani wa tani 2,193.3 kwa mwaka.

“Kutokana na kiwango hiki cha uzalishaji, Rais aliona umuhimu wa kuwa na kiwanda cha kukoboa kahawa katika eneo hili,” amesema Londo.

Ameeleza kuwa Serikali, kupitia Halmashauri ya Nyasa, imetenga eneo lililopo Kitongoji cha Ndanda, Kijiji cha Kingiritiki, Kata ya Kingiritiki, kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho.

Kwa mujibu wa Londo, eneo hilo lina ukubwa wa hekta nne (sawa na ekari 10) na lina miundombinu wezeshi ikiwemo barabara, maji na umeme.

“Eneo hili linamilikiwa na Serikali na lipo tayari kwa mwekezaji yeyote atakayejitokeza kujenga kiwanda cha kukoboa kahawa. Serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji kuwekeza katika eneo hilo,” amesisitiza.

Katika swali la nyongeza, Mbunge Nchimbi amehoji kwa nini Serikali isianze moja kwa moja utekelezaji wa mradi huo badala ya kusubiri wawekezaji kutoka sekta binafsi, hali inayochukua muda mrefu.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri Londo amesema utekelezaji tayari umeanza, ambapo miche ya kahawa milioni mbili imetolewa kwa wakulima, hatua iliyoongeza uzalishaji wa zao hilo.

“Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhamasisha uwekezaji ili kujenga uchumi jumuishi utakaoleta manufaa kwa wakulima wa kahawa nchini,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button