Spika ahoji TCRA, CMSA

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu, ameziagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kufika mbele ya Kamati ya Bajeti ya Bunge kutoa maelezo kuhusu kutotekelezwa kwa sheria inayozitaka kampuni za mawasiliano kuuza sehemu ya hisa zao kwa umma.

Maelekezo hayo yametolewa leo bungeni baada ya Spika kuhoji sababu zilizoifanya kampuni ya Vodacom Tanzania kuwa pekee iliyotekeleza takwa hilo la kisheria, huku kampuni nyingine za mawasiliano zikiendelea kutofanya hivyo licha ya kuwepo kwa sheria husika.

Akizungumza bungeni, Zungu amesema lengo la sheria hiyo ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na kuwapa Watanzania fursa ya kumiliki hisa katika makampuni ya mawasiliano. Hata hivyo, ameeleza kusikitishwa na utekelezaji hafifu wa matakwa hayo, akisisitiza kuwa TCRA, kama msimamizi wa sekta hiyo, inapaswa kuchukua hatua kuhakikisha sheria inazingatiwa.

“Hadi hivi sasa ni kampuni moja tu ya Vodacom imeweza kutekeleza masharti hayo ya kisheria ya kuuza hisa kwa umma na kuongeza uwazi wa uwajibikaji wa makampuni hayo. Jambo la kujiuliza ni kwa nini TCRA hawajachukua hatua za makusudi kuhakikisha takwa hilo linatekelezwa,” amesema Zungu.

Spika huyo pia amehoji jukumu la CMSA katika kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo na kuagiza mamlaka hizo mbili kukutana na Kamati ya Bajeti kueleza kwa nini hoja zilizobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hazijafanyiwa kazi. SOMA: TCRA yahimiza umakini kulinda amani, umoja

Aidha, ameonya kuwa Serikali inaendelea kupoteza mapato kutokana na kutotekelezwa kwa sharia akitolea mfano nchi nyingine hupata mapato makubwa kupitia gawio la kampuni za simu zinazouza hisa kwa umma. Vodacom Tanzania iliorodhesha hisa zake katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mwaka 2017 na hadi sasa ndiyo kampuni pekee ya mawasiliano iliyotekeleza sharti hilo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button