TCRA yahimiza umakini kulinda amani, umoja

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema ni muhimu vyombo vya habari na wananchi walinde umoja, amani na mshikamano wa taifa, kwa kuzuia maudhui yasiyofaa kwa jamii.

Akiwa Dar es Salaam, Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji TCRA, Andrew Kisaka amesema ni muhimu wananchi wafute taarifa za kizushi na wajiepushe kuzisambaza.

Kisaka amesema kumekuwa na watu wanaosambaza taarifa za kizushi mtandaoni, hasa zinazoweza kuchochea taharuki na kuvuruga amani.

Amehimiza watangazaji wazingatie kanuni za utangazaji zinazohusu kampeni za siasa wakati wa Uchaguzi Mkuu kwa kupata taarifa kwenye vyanzo rasmi na kuzingatia mizania kabla ya kutangaza au kusambaza habari hizo.

SOMA: TCRA waanzisha kampeni ulinzi mitandaoni

Kisaka amesema Kampeni ya TCRA ya ‘Futa Delete Kabi sa’ inamuwezesha mwananchi kuepuka madhara ya kuchukuliwa hatua za kisheria yanayotokana na kusambaza taarifa potofu.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma TCRA, Rolf Kibaja amesema kwa sasa kuna usambazaji wa taarifa za uzushi zinazotengenezwa kwa kutumia akili unde.

“Unaweza kutumia teknolojia saidizi kubaini uhalisia wa taarifa ya picha, ikiwemo uchapaji wake wa mara ya kwanza au kwa kuangalia viashiria kama vile takwimu zisizo sahihi, makosa ya kisarufi au majina na kuwa na vihisishi vingi vyenye kuongeza chumvi,” amesema Kibaja.

Ofisa Mhifadhi Mwandamizi wa TCRA, Raphael Mwango amesema kizazi cha sasa kinafikiwa na taarifa kwa haraka, tofauti na zamani.

Mwango amesema vijana wengi huanza kutumia simu janja mapema, hali inayowapa fursa ya kupata taarifa nzuri na potofu.

Amesema kampeni ya TCRA ni jibu la kimkakati kukabili changamoto za taarifa potofu, huku ikilenga kuwasaidia vijana na wazazi kujilinda kisheria.

Mwango amesema uzushi unaweza kuathiri afya ya akili, kuvuruga mshikamano wa wananchi, kuharibu heshima ya mtu au hata kuchangia vifo.

Amesema kampeni hio itatekelezwa kwa muda wa miezi sita na akasema TCRA imejipanga kukabili changamoto hiyo kwa kuwahamasisha wananchi kutumia teknolojia kwa uangalifu na kufuata taratibu zilizo sahihi.

Ametoa mwito kwa wananchi wawe makini na taarifa wanazopokea au kusambaza mtandaoni na akasema taarifa kuhusu matokeo ya uchaguzi zisizotolewa na mamlaka zinaweza kusababisha migogoro na taharuki isiyo ya lazima.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button