Maadhimisho siku ya saratani yatoa tumaini

DAR ES SALAAM: MAADHIMISHO ya Siku ya Saratani Duniani yamewapa matumaini wananchi na wanusurika wa ugonjwa wa saratani, kufuatia kuimarika kwa ushirikiano kati ya Serikali, wataalamu wa afya na wadau mbalimbali katika juhudi za kuzuia, kugundua mapema na kudhibiti ugonjwa huo.
 
Maadhimisho hayo kitaifa yamefanyika leo Februari 4, katika viwanja vya Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dar es Salaam ikihusisha wadau mbalimbali ikiwemo Taasisi ya GSM Foundation.
 
Tukio hilo limewakutanisha viongozi wa Serikali, wataalamu wa afya, mashirika ya kiraia, sekta binafsi pamoja na wananchi, likiwa na lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu saratani na kuhimiza uchunguzi wa mapema kama njia ya kupunguza madhara ya ugonjwa huo.
 
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa GSM Foundation, Faith Gugu amesema ushiriki wa taasisi hiyo ni sehemu ya dhamira ya muda mrefu ya kuchangia uboreshaji wa afya ya jamii, hususani kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.

Faith alisema uzoefu uliopatikana kupitia kambi za matibabu zilizotekelezwa kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Amana unaonesha bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu sahihi ya afya na uhamasishaji wa jamii.

“Wananchi wengi huchelewa kufika vituo vya afya kutokana na ukosefu wa taarifa za mapema, hali inayoongeza madhara ya saratani kwa kufika kwenye vituo vya afya wakiwa katika hatua za juu za ugonjwa,” amesema Faith.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Ocean Road, Dk Diwani Msemo amesema ugonjwa wa saratani unaweza kuzuilika kwa asilimia 80 kwa kupata chanjo na asilimia 20 kwa kufanya uchunguzi wa awali na utambuzi wa mapema.

Awali, akieleza hayo Dk Msemo amesema ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi umekuwa ikiendelea kuongoza kwa asilimia 23 takribani miaka 10, ikifuatiwa na saratani ya matiti, saratani ya utumbo Mpana na ya tezi dume kwa wanaume.

“Katika nchi zilizoendelea ni kama vile ugonjwa huu haupo kwa sababu watu wamechanja na wanaendelea kufanya uchunguzi kwa ambao hawakuchanja,” amesema Dk Msemo.

Katika kuonesha mshikamano wa kijamii, taasisi hiyo imefanikisha shughuli mbalimbali ikiwemo matembezi ya hisani, uchunguzi wa awali wa saratani, utoaji wa elimu ya saratani pamoja na zoezi la uchangiaji wa damu, hatua iliyolenga kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa huduma za afya.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button