Sayansi kupewa nafasi kuthibitisha tiba asilia

DAR ES SALAAM: Serikali imeongeza msukumo wa kuunganisha tiba asilia na tiba za kisasa kwa kuwataka wanasayansi na wataalamu wa afya nchini kutumia mbinu za kisayansi kuthibitisha ufanisi wa maarifa ya tiba za jadi zinazotumiwa na wananchi kabla ya kuziingiza katika mfumo rasmi wa huduma za afya.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua Mkutano wa 14 wa Kisayansi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema tiba asilia zinapaswa kufanyiwa utafiti wa kina, majaribio ya kitabibu (clinical trials) na tathmini za kitaalamu ili kubaini usalama, ufanisi, dozi sahihi na matumizi yake kwa makundi mbalimbali ya wagonjwa.

Alisisitiza kuwa dhamira ya serikali si kuondoa au kudharau tiba asilia, bali kuiboresha na kuipa nguvu kupitia sayansi ili iweze kutumika kwa usalama ndani ya mfumo wa afya wa kisasa. Alisema ni wajibu wa sayansi kuchunguza, kuthibitisha na kubaini ukweli wa madai yote ya tiba, iwe ya kisasa au ya jadi, kupitia mbinu madhubuti za utafiti.
“Tunapochunguza madai ya ufanisi, iwe kutoka tiba asilia au nyinginezo, jukumu la sayansi liko wazi, kupima, kuthibitisha na kuanzisha ukweli kupitia mbinu madhubuti,” alisema. Prof. Mkenda. Alisisitiza kuwa lengo si kukataa tiba asilia, bali kuiinua kupitia sayansi na kuhakikisha matumizi yake salama ndani ya huduma za afya za kisasa.

Prof. Mkenda alieleza kuwa serikali itaanzisha mashauriano ya kitaifa yatakayowakutanisha watafiti, waganga wa tiba asilia, wasimamizi wa sekta ya afya pamoja na wataalamu wa haki miliki ili kuweka mfumo wa pamoja wa tathmini, uthibitisho na ulinzi wa maarifa ya tiba asilia. Alionya kuwa bila uthibitisho wa kisayansi, matumizi ya tiba zisizojaribiwa yanaweza kuhatarisha afya za wananchi.
Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alisema chuo hicho kinawekeza katika teknolojia za kisasa zikiwemo akili bandia (AI), genomiki na uchunguzi wa molekuli ili kuimarisha utafiti na utoaji wa huduma za afya.

Alisema kuanzishwa kwa huduma za “next-generation sequencing” kumeiwezesha MUHAS kuwa kitovu cha kikanda katika tafiti za jeni na tiba maalum (precision medicine), hatua itakayosaidia kuchambua kwa kina magonjwa na kutathmini tiba mbalimbali, ikiwemo zinazotokana na maarifa ya tiba asilia.
Prof. Kamuhabwa aliongeza kuwa vyuo vikuu vinapaswa kwenda zaidi ya kuchapisha tafiti pekee na badala yake kuleta suluhisho zinazogusa moja kwa moja changamoto za afya za wananchi na kuboresha mifumo ya huduma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Kisayansi MUHAS, Prof. Raphael Sengeja, alisema mkutano huo umeendelea kukua ambapo mwaka huu jumla ya maudhui 247 ya utafiti yaliwasilishwa, yakiwemo mawasilisho 138 ya mdomo na mabango 109 ya kisayansi.
Alisema tafiti hizo zinahusisha maeneo mbalimbali ikiwemo tiba asilia, akili bandia, genomiki, afya ya uzazi, usugu wa dawa dhidi ya bakteria pamoja na uimarishaji wa mifumo ya afya. Alisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha utafiti unabadilika na kuwa suluhisho la moja kwa moja kwa jamii badala ya kubaki kwenye majarida ya kitaaluma pekee.
Kwa ujumla, mkutano huo umeonesha mwelekeo wa taifa wa kuimarisha ushirikiano kati ya tiba asilia na sayansi ya kisasa, huku msisitizo ukiwekwa kwenye uthibitisho wa kisayansi, usalama wa wagonjwa na matumizi endelevu ya maarifa ya ndani katika kuboresha afya ya jamii.




https://youtu.be/E6RH8ylJxps?si=6RBUidOu85-yH9Fe
https://youtu.be/zvG5y2XeXLA?si=CdQeTIYYmG9SVQaB
https://youtu.be/iah3kkD5Zf4?si=H1fpNw10GWa1LO_f
https://youtu.be/_yzsR0Fw_aw?si=aPMhbCR_AnqD00jk
https://youtu.be/V6IjRJWpS4c?si=-8HLLDri8YPhha2X