Serikali kuweka nguvu utumishi wenye uadilifu

MOROGORO: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimanti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kutimiza dhamira yake ya kuujenga utumishi wa umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa wananchi.
Ridhiwani amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa mamkala za maji nchini kuhusu utekelezaji wa sheria ya utumishi wa umma Sura 298 ( Marejeo ya Mwaka 2023) na matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia rufaa na malalamiko, na uwasilishaji wa taarifa za kiutumishi kwa Tume ya Utumishi wa Umma.

Amesema, ofisi yake itaendelea kuisimamia na kuisaidia tume hiyo kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kisheria ili iweze kuujenga utumishi wa umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa wananchi kwa kutoa huduma bora.
Mbali na hayo amesema tume katika kutekeleza majukumu yake imebaini kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi katika usimamizi na uendeshaji wa masuala ya rasilimali watu kwenye baadhi ya mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira nchini.
Amesema takwimu zinaonesha kati ya rufaa 52 zilizopokelewa kutoka mamlaka za maji na kutolewa uamuzi na tume kupitia mikutano yake kwa kipindi ya miaka ya fedha 2023/2024, 2024/2025 hadi Desemba 2025.

Waziri amesema rufaa 20 sawa na asilimia 38 ya rufaa zote zilizopokelewa katika kipindi hicho zilionekana kuwa na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma .
Amesema kutokana na ukiukwaji huo kumeifanya tume kuzirudisha ili mchakato wa mashauri ya kinidhamu ianze upya au warufani kufutiwa hatia na kurejeshwa kazini.
Kutokana na ukiukwaji huo, ameziagiza mamlaka zote za nidhamu nchini zikiwemo za mamlaka za maji kusimamia na kuzingatia ipasavyo sheria, kanuni na taratibu katika usimamizi na uendeshaji wa Masuala ya Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma ili kuiepushia Serikali hasara zisizo za lazima.
Waziri huyo pia amewataka waajiri, mamlaka za ajira na mamlaka za nidhamu nchi nzima kuwasilisha vielelezo vya rufaa na malalamiko tume kwa wakati kama sheria inavyoelekeza pale zinapotakiwa kufanya hivyo.
Amesema Mamlaka ambazo hazitazingatia maelekezo hayo, Serikali haitasita kuchukua hatua za nidhamu dhidi yao.
Pia ameipongeza Tume kwa kujenga Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia Rufaa na Malalamiko katika Utumishi wa Umma na Uwasilishaji wa Taarifa za Kiutumishi Tume (PSCMIS).
“Uwasilishaji wa taarifa za kiutumishi za kila Robo Mwaka kupitia ujazaji wa Fomu mbalimbali,kwa sasa taarifa hizo zitakuwa zinatumwa kupitia Mfumo na hili ni jambo la kujivunia,”amesema Ridhiwani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola amesema sheria, kanuni na taratibu zinapokiukwa zinasababisha baadhi ya rufaa kurudishwa na kuchelewesha mambo yakiwemo ya haki ya mtumishi wenye kutumiwa kutopatikana kwa wakati..
“Kwa niaba ya tume inaikukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuiwezesha kibajeti na kuisaidia kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi na hivyo kuboresha usimamizi wa utumishi wa umma na kuboresha huduma zinazotolewa kwa watanzania,” amesema Jaji mstaafu Kalombola.



