Mambo 5 yatajwa tija mikopo ya asilimia 10

WATAALAMU wa uchumi wameshauri mambo matano yazingatiwe ili kuongeza ufanisi wa mikopo ya asilimia 10 inayotengwa na halmashauri.

Serikali inatoa mikopo ya asilimia 10 kupitia mgawanyo wa asilimia nne vijana, asilimia nne wanawake na asilimia mbili wenye ulemavu kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

Wataalamu hao wametaja elimu ya usimamizi wa fedha na kufahamu maeneo sahihi ya kuwekeza fedha hizo kuwa kati ya mambo hayo.

SOMA: Mvomero wafanya kweli mikopo asilimia 10

Mtaalamu wa uchumi, Profesa Kitojo Wetengere alisema wote wanaohusika katika mchakato huo wanapaswa kuwa na mtazamo sahihi kama kweli mtaji ndiyo changamoto ya vikundi hivyo.

“Hao wanaokopa wajue kabisa je tatizo lao ni mtaji au ni nini, mikopo inatolewa kwenda kutatua tatizo la mtaji sasa kutokujua kama tatizo ni mtaji lakini wanatoa mtaji ndio inatufanya tushindwe kusonga mbele kutoka hapa,” alisema Profesa Watengere.

Alisema ni muhimu kuwa na nidhamu ya fedha ili wahusika wanapopata fedha wasitumie katika starehe na mambo mengine ambayo hayakuwa katika malengo sahihi ya fedha hizo.

Mhadhiri wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Mwanza, Damas Mushi alisema kikundi kinapochukua mkopo kihakikishe wote wanaaminiana na wana malengo yanayofanana ili asiwepo wa kuwarudisha nyuma wengine na hatimaye kujikuta wakipata hasara.

Mushi alipendekeza vikundi hivyo vifanye utafiti wa wanachotarajia kwenda kufanya na viombe ushauri wa matumizi sahihi za mikopo hiyo kwa maofisa biashara wa halmashauri.

Rais wa Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA), Godvictor Lymo alisema vikundi hivyo ni vizuri kuwa na elimu ya usimamizi na utunzaji wa fedha wanazopata na kutambua wanapaswa kuzalisha ili wapate faida na kurejesha mikopo.

Lyimo alisema elimu ya kusimamia fedha itawafundisha wanufaika mambo mengi ikiwamo nidhamu ya fedha, dondoo za namna sahihi ya kutunza fedha na kukuza mtaji.

“Halmashauri inaweza ikawa inafanya kama ubia kwa mfano na Chama cha Wahasibu Tanzania, mfano wakawaambia tuna vikundi 20 tunategemea kuvikopesha tunaomba mvinoe wajue jinsi gani ya kutunza fedha, nidhamu, kukuza mitaji, kukuza mradi vizuri na usimamizi halafu wakimaliza pale wanakuwa kama wanapewa uthibitisho na inakuwa sehemu ya kigezo cha kupewa mkopo,” alibainisha Lyimo.

Pia, alipendekeza vikundi hivyo vinapoenda kuomba mikopo viandae andiko linaloeleza wazi kile wanachokwenda kufanya ikihusisha namna wakakavyopata faida.

“Utaratibu uwe kama wa benki, unapokwenda kukopa benki lazima uwe na andiko lako ambalo litaonesha kabisa kama ni biashara unaombea mkopo, je ni biashara gani unakwenda kufanya na je inatushawishi kwamba huu mkopo utaenda kuzaa ukunufaishe wewe na uweze kurejesha,” alieleza Lyimo.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button