Vituo 23 vya kukusanyia maziwa vyazinduliwa

KAGERA: Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), na Serikali imezindua rasmi vituo 23 vya kukusanyia maziwa (Milk Collection Centers – MCCs) vilivyojengwa na kuboreshwa kupitia Mradi Shirikishi wa Wasindikaji na Wazalishaji wa Maziwa Tanzania (TI3P).
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Bashiru Ally amesema mradi wa TI3P utaleta mageuzi makubwa katika mnyororo wa thamani wa maziwa nchini kwa kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa maziwa na kupanua masoko kwa wafugaji wadogo, wa kati na wakubwa huku.

Alisema Mkoa wa Kagera uliwahi kupiga hatua kwa kujikita katika maswala ya ushirika na baadaye wakaanguka, ambapo amedai kuwa kufufua ushirika huu kwa njia ya ufugaji ni njia ambayo inaweza kuwainua pia katika ngazi ya kaya na kuurudishia mkoa hadhi yake ya uchumi kama miaka iliyopita.
Aidha, aliwashuri wafadhili wa mradi wa TI3P, Shirika la Gates Foundation na watekelezaji wa mradi huo TADB kwa kushirikiana mashirika Heifer International Tanzania na LandO’lakes Venture 37, ukiwa na lengo la kuwaunganisha wazalishaji na wasindikaji ili kukuza sekta ya maziwa kwa njia jumuishi na endelevu maarufu kama kopa ngo,mbe lipa maziwa.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema hadi sasa mradi umewezesha Zaidi ya Sh bilioni 41 kutolewa kama mikopo kwa wadau katika mnyororo wa thamani wa maziwa.
Alisema mradi huo umewezesha Ununuzi wa mitambo 3,254 yenye thamani ya Sh bilioni 10.8 kwa lengo la kuongeza uzalishaji pamoja na ufadhili wa viwanda 15 vya usindikaji maziwa kwa Sh bilioni 22.

Alisema wafugaji 92,831 watafikiwa moja kwa moja kupitia huduma za kifedha, mafunzo na ugani,
Ruzuku fungamanifu ya Sh bilioni 1.448 kutolewa kwa wafugaji na wasindikaji wa maziwa,Kuanzishwa na kuimarishwa kwa Vyama vya Wazalishaji wa Maziwa (FPOs) 45 vinavyokusanya wastani wa lita 19,047 kwa siku.
Ujenzi na uboreshaji wa vituo 23 vya kukusanyia maziwa katika Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar, vyenye uwezo wa kukusanya lita 45,500 kwa siku na kuhudumia wafugaji 4,016 katika mikoa 8 na wilaya 18, kwa uwekezaji wa zaidi ya Sh bilioni 1.157.

Katika ziara ya waziri wa mifugo mkoani Kagera alitembelea Chama cha Ushirika cha Maruku, Bukoba Mjini, ambapo alishuhudia utekelezaji wa mpango wa “Kopa Ng’ombe, Lipa Maziwa” unaolenga kuongeza kipato kwa vijana na wanawake kupitia ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa.
Kupitia chama hicho chenye wanachama 118 (asilimia 26 wanawake), wanachama 24 wamenufaika na mitamba 24 yenye mimba. Pia wamepata ruzuku ya Sh milioni 18 kupunguza marejesho ya mikopo, ukarabati wa MCC wenye thamani ya Sh milioni 10.4 pamoja na tanki la kuhifadhia maziwa la lita 2,000.
Wanachama hao pia wamepatiwa mbegu bora za malisho aina ya Juncao na mafunzo ya ufugaji bora kutoka Heifer International.
Katika Kituo cha Nshamba, chenye wanachama 541 (wanawake 83), TADB imewezesha uanzishwaji wa MCC yenye uwezo wa kukusanya lita 2,000 kwa siku pamoja na jenereta ya dharura. Wanachama 143 wako katika mchakato wa kunufaika na mpango wa “Kopa Ng’ombe, Lipa Maziwa” kwa kupatiwa mitamba 45 yenye mimba.
Aidha, katika Ushirika wa UWAWAMA, Kayanga wilayani Karagwe, wanachama 76 wamenufaika na mpango huo kwa kupatiwa mitamba 110 yenye mimba na ruzuku ya Sh milioni 85 ya kupunguza marejesho ya mikopo.



