Tume ya uchunguzi yakutana na Abdurahman Kinana

TUME ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, jana Machi 2, 2026 imekutana na mwanasiasa mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.
Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Tanganyika uliopo kwenye jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Tume kukusanya taarifa, maoni na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu, viongozi wa sasa na wastaafu pamoja na wananchi wa kawaida.

Katika kikao hicho, hoja zilizojadiliwa zilihusu tathmini ya athari za matukio hayo ndani na nje ya nchi, pamoja na ushauri wa hatua za kijamii na kisheria zinazoweza kuchukuliwa ili kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa. SOMA: Tume,Mufti wateta matukio ya Oktoba 29
Tume hiyo inaendelea na mahojiano na waathirika wa matukio hayo baada ya hivi karibuni Mamlaka ya Uteuzi kuiongezea muda wa siku 42 kuanzia Februari 20, 2026 ili kukamilisha uchunguzi wake. Tume inatarajiwa kuwasilisha taarifa yake kabla au ifikapo Aprili 3, 2026.



