Kazi zenye staha zajadiliwa Morogoro

WAKATI sekta ya sanaa na ubunifu ikiendelea kukua kwa kasi na kutoa ajira kwa maelfu ya vijana nchini, wadau wameonya kuwa bila kuwepo kwa kazi zenye staha, mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa unaweza kubaki kwenye takwimu zisizogusa maisha halisi ya wasanii.
Kauli hiyo imetolewa katika warsha ya siku tatu ya kusambaza matokeo ya utafiti kuhusu uendelezaji wa kazi zenye staha katika sekta ya utamaduni na uchumi wa ubunifu nchini Tanzania. Warsha hiyo imeandaliwa na Shirika la Kazi Duniani kwa ufadhili wa Norway.
Utafiti uliowasilishwa umebainisha kuwa licha ya sekta ya utamaduni na ubunifu kuongeza mchango wake katika pato la Taifa na ajira kwa vijana, ukuaji huo haujaambatana na ulinzi wa kijamii, mikataba rasmi wala mazingira salama ya kazi kwa wasanii wengi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Taasisi ya SEDEVA, Izack Abeneko, amesema pamoja na sekta hiyo kuwa chanzo kikubwa cha kipato na ajira hasa kwa vijana, bado kuna haja ya kuweka mifumo madhubuti ya kulinda haki za wasanii na kurasimisha shughuli zao.
“Mazingira ya kazi ya wasanii wengi bado si rasmi. Ni kazi za msimu au za hapa na pale; msanii hawezi kujua ni lini atapata kazi nyingine. Serikali inapaswa kuimarisha utekelezaji wa sheria zilizopo ili zilete matokeo chanya kwa wadau wa sanaa na kumpunguzia mzigo msanii huku akielewa thamani ya kulinda haki zake,” amesema Abeneko.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Masoko wa Baraza la Sanaa la Taifa, Mrisho Mrisho, amesema warsha hiyo imeibua maeneo matatu muhimu yanayohitaji kupewa kipaumbele. “Kwanza ni suala la kazi zenye staha katika sekta ya sanaa, pili ni mfumo wa kisheria na sera, na tatu ni mapato ya wasanii. Tunahitaji kuona namna bora ya kurasimisha sekta katika maeneo hayo,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, Dk. Kassim Kapalata, amesisitiza umuhimu wa wasanii kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kulinda maslahi yao. SOMA: ZMBF Yapongeza Sanaa na Ubunifu Sharjah
Wadau wamehitimisha kuwa utekelezaji wa mapendekezo ya utafiti huo utakuwa hatua muhimu katika kuhakikisha sekta ya sanaa na utamaduni inachangia kwa tija zaidi uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.



