SMZ kuboresha usafiri wa anga

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeeleza mikakati ya kuimarisha usafiri wa anga ikiwamo kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Pemba. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed amesema hayo wakati akitoa taarifa kuhusu mafanikio ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika siku 100 madarakani juzi.
“Uwanja wa Ndege wa Pemba unajengwa sasa hivi kupitia Kampuni ya Propav wanajenga jengo la abiria na wameanza kuongeza urefu wa njia ya kutua na kurukia ndege iliyokuwepo ni kilometa 1.5 tunataka kuongeza kuwa 2.5,” alieleza Dk Mohamed.
Ameongeza: “Sasa tunaiunganisha Pemba katika ‘circuit’ (mlolongo) ya utalii kwa maana watalii wanaweza kutoka Kenya moja kwa moja wakaja Pemba na tayari katika siku 100 tumejenga meta 600 upande wa Kaskazini katika kuongeza urefu wa ule njia ya kurukia”.
Amesema wamekamilisha ujenzi wa sehemu maalumu kwa viongozi mashuhuri na jengo hilo limekamilika na litazinduliwa hivi karibuni na ina mpango wa kujenga jengo la nne la nne la abiria ili kuongeza uwezo wa kubeba abiria.
Amesema tangu Novemba 2025 hadi Februari 2026, idadi ya abiria imefikia 878,698 na matarajio hadi kufikia Desemba 2026 abiria watafikia milioni 3.3 hadi 3.5 hivyo mahitaji ya jengo la abiria ni muhimu.
Dk Mohamed amesema chini ya uongozi wa Dk Mwinyi wamefanya maboresho katika ujenzi wa karakana kuu ya matengenezo ya ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Abeid Aman Karume itakayokuwa na vifaa vya kuwezesha ndege za mataifa jirani kufanyiwa matengenezo katika karakana hiyo na tayari wawekezaji watatu wameonesha nia ya kuijenga.
Kando na karakana hiyo, pia katika siku 100 za Dk Mwinyi, Dk Mohamed amesema matayarisho ya ujenzi wa mnara mpya wa kuongozea ndege uliopo katika hatua ya usanifu mchoro umeanza. Mafanikio mengine katika siku 100 za Dk Mwinyi wizara imekamilisha ujenzi wa jengo la biashara kwa asilimia 90 lengo la kutanua wigo wa utoaji huduma za kibiashara lililojumuisha maduka, ofisi na migahawa.
Pia, Dk Mohamed ameeleza kuwa ujenzi wa vituo viwili vya mafuta ya ndege unaendelea kwa lengo la kuongeza idadi kufikia vinne ili kuongeza ushindani, kuboresha huduma na kujihakikishia upatikanaji wa mafuta ya ndege nchini. SOMA: Masauni ahimiza wanafunzi Zanzibar kulinda, kuenzi Muungano
Ameeleza kuwa ujenzi wa maegesho ya ndege unaendelea katika siku 100 za Dk Mwinyi yanayojengwa chini ya Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) pamoja na ujenzi wa kituo cha kuhifadhia mizigo. Pia, wameanza matayarisho ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Nungwi kitakachokuwa cha kimataifa.



