Wajishindia mil 17 na kuinua uchumi wao

Wajasiriamali watatu wenye ulemavu wamejishindia jumla ya Sh milioni 17 kama mtaji wa kuendeleza biashara zao baada ya kuibuka washindi katika mashindano ya Wazo Bora Pitch yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yaliwashirikisha wajasiriamali 15 waliopitia mafunzo maalumu ya kuboresha mifumo ya biashara, usimamizi wa fedha pamoja na maandalizi ya kupata uwekezaji.

Katika matokeo ya mashindano hayo, Ng’oga Kaswahili aliibuka mshindi wa kwanza na kujishindia Sh milioni 10 kama mtaji wa biashara.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Mohamed Muhidini aliyepata Sh milioni 4, huku Nipaeli Mtana akishika nafasi ya tatu na kujishindia Sh milioni 3.

Akizungumza na HabariLEO katika hafla ya kuwatangaza washindi hao, Mtendaji Mkuu wa Standard Chartered Bank Tanzania, George Binde, alisema msaada uliotolewa Desemba mwaka jana umeanza kuonesha matokeo chanya kwa kuwawezesha wajasiriamali kuimarisha biashara zao.

Amesema washiriki wa programu hiyo wameonesha maendeleo makubwa katika kuendesha biashara zao kwa ubunifu, uthubutu na uthabiti katika kuendeleza mawazo yao ya biashara.

“Mtaji wa Sh milioni 17 uliotolewa utasaidia kupanua biashara, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa soko kwa biashara zilizoshinda,” amesema Binde.

Mashindano ya Wazo Bora Pitch yalianza Desemba 2025 baada ya Standard Chartered Bank Tanzania kutoa msaada wa dola za Marekani 11,500 kwa Challenges Worldwide Tanzania ili kusaidia kukuza ujasiriamali na uchumi jumuishi.

Baada ya kufungwa kwa dirisha la maombi, washiriki 15 walichaguliwa kushiriki mafunzo maalumu ya kukuza uwezo wa biashara zao. Mwishoni mwa mafunzo hayo, washiriki saba walifanikiwa kufika hatua ya mwisho na kuwasilisha mawazo yao ya biashara mbele ya majaji katika tukio la mwisho lililofanyika Dar es Salaam.

Mpango huo unatekelezwa na Challenges Worldwide Tanzania kwa ufadhili wa Standard Chartered Bank Tanzania kupitia programu ya RISE/E ya Standard Chartered Foundation inayolenga kuwawezesha wajasiriamali kukuza biashara zao na kuimarisha uchumi jumuishi.

Programu hiyo ya miaka mitatu yenye thamani ya Sh bilioni 2.2, iliyoanzishwa mwaka 2024, inalenga kusaidia moja kwa moja biashara ndogo 340 pamoja na kutengeneza ajira mpya 478 nchini, huku ikiwalenga zaidi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika hafla hiyo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum anayewakilisha watu wenye ulemavu, Yumna Mmanga, alipongeza mpango huo akisema unachangia kukuza ushiriki jumuishi wa kiuchumi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Amesema vipaji na ubunifu havibagui jinsia wala ulemavu, hivyo ni muhimu kuendelea kuweka mazingira yanayowezesha makundi hayo kupata fursa sawa za kuendeleza mawazo yao ya biashara.

Mmanga ameongeza kuwa jitihada hizo zinaendana na maono ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha uwezeshaji wa kiuchumi jumuishi kwa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Youth with Disability Organization (YOWDO), Rajabu Mpilimpili, amesema wanafurahia kuwa sehemu ya mchakato wa mashindano hayo kwa kushirikiana na Challenges Worldwide Tanzania pamoja na Standard Chartered Bank Tanzania katika kuwawezesha watu wenye ulemavu kujiajiri kupitia ubunifu wa mawazo yao ya biashara.

Amesema mashindano ya Wazo Bora yamekuwa jukwaa muhimu la kuonesha ubunifu na uwezo wa watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kiuchumi na kijamii nchini.

“Mashindano haya yanaonesha wazi kuwa watu wenye ulemavu wana uwezo mkubwa wa kuwa wabunifu na wachangiaji muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania,” amesema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button