Wanawake wahimizwa kupima afya mapema

KATIKA kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, wanawake wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao mapema, hususan kwa magonjwa yanayoathiri zaidi kundi hilo kama saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake yaliyofanyika katika Hospitali ya Dar Group jijini Dar es Salaam, Meneja Rasilimali Watu wa kampuni ya Said Salim Bakhresa Group, Mwanafumo Mohammed amesema ni muhimu wanawake kupima afya zao mapema ili kubaini magonjwa kabla hayajafikia hatua mbaya.

Amesema hivi sasa huduma za afya zinapatikana katika hospitali mbalimbali, na wakati mwingine hutolewa bure, hivyo wanawake wanapaswa kutumia fursa hiyo kujua hali ya afya zao. “Nimetembelea maeneo mbalimbali na nimeona wanawake wakijitokeza kuchunguza afya zao. Hata hivyo, bado tunahitaji kuhamasisha zaidi wanawake kupima mapema magonjwa kama saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya matiti, magonjwa ya moyo na mengineyo,” alisisitiza.

Ameongeza kuwa Hospitali ya Dar Group ina huduma bora na vifaa vya kutosha kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, lakini bado mahitaji ni makubwa kutokana na idadi ya watu wanaohudumiwa. Kwa hiyo ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana na hospitali hiyo katika juhudi za kupanua huduma zake ili iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.

“Siku ya Wanawake ni muhimu sana, na imekuwa fursa ya kufanya mambo mengi ya maendeleo. Tunahitaji pia kutoa ushirikiano katika kuimarisha taasisi za afya kama Hospitali ya Dar Group,” alisema. SOMA: Mkurugenzi Mtendaji TSN asifu mchango wanawake

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake wa Hospitali ya Dar Group, Grace Mkama amesema katika maadhimisho hayo wamefanikiwa kutoa huduma ya upimaji wa magonjwa mbalimbali ikiwemo presha, kisukari, saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti kwa wanawake zaidi ya 250. Amesema mwitikio wa wanawake kujitokeza kupima afya zao ulikuwa mkubwa kutokana na kuongezeka kwa magonjwa hayo katika jamii.

“Mwitikio ulikuwa mkubwa sana kwa sababu magonjwa haya yanaathiri wanawake wengi. Tunawashauri wanawake kujitokeza kila wanaposikia kuna huduma za upimaji bure, lakini hata kama hakuna, waende hospitali zilizopo karibu nao kupima afya zao mara kwa mara kwani wao ndio walezi wakuu wa familia,” alieleza.

Naye Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Hospitali ya Dar Group, Abdulrahman Muya, akimwakilisha Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Tulizo Shemu, amesema taasisi hiyo imeungana na wanawake kupitia umoja wao kutoa huduma mbalimbali kwa jamii. Amesema huduma hizo ni pamoja na kusaidia wahitaji, kuwahudumia wagonjwa na kutoa huduma za upimaji wa afya kwa wanawake.

“Maadhimisho haya yametukumbusha umuhimu wa umoja na ushirikiano katika jamii. Kupitia kaulimbiu ya mwaka huu inayozungumzia haki, usawa na ujumuishaji kwa wanawake na wasichana kuelekea Dira ya Maendeleo ya 2050, sisi kama taasisi tumeona ni muhimu kushirikiana na sekta binafsi kama Bakhresa Group ili kuimarisha huduma kwa jamii,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button