Mkurugenzi Mtendaji TSN asifu mchango wanawake

DAR ES SALAAM: Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Asha Dachi, amepongeza kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na maendeleo ya taifa, akisema mchango wao unaendelea kukua katika sekta mbalimbali za uchumi.
 
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 6, 2027 kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika Machi 8, Mkurugenzi huyo amesema TSN ilianza shughuli zake za ndani za kuadhimisha siku hiyo tangu Machi 1 kwa kuendesha mafunzo mbalimbali katika makao makuu ya taasisi hiyo yaliyopo Tazara.
 
Aidha, alisema katika kuadhimisha siku hiyo muhimu, wanawake wa kampuni hiyo walikata keki kama ishara ya kutambua mchango wa wanawake na hatua iliyofikiwa kuelekea uwiano wa usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50, akibainisha kuwa kwa sasa wanawake wamefikia takribani asilimia 30 katika vyombo vya uwakilishi.
 
“Tunajivunia mafanikio tuliyoyapata hadi sasa. Wanawake wanaendelea kuonesha weledi na kuaminika katika utendaji wao wa kazi,” alisema.
 
Pia, aliusifia uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan akisema kuwa umekuwa chachu kubwa katika kuhamasisha wanawake kujitokeza na kushika nafasi za uongozi pamoja na kushiriki kikamilifu katika sekta mbalimbali.
 
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, wanawake wanaonekana zaidi katika sekta mbali mbali kama madini, utalii, afya, elimu pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi, ambako wanaendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya taifa.
 
Alisema kaulimbiu ya mwaka huu inayosema, “Haki Sawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050,” inaonesha umuhimu wa kuweka mazingira ya fursa sawa kwa wanawake na wasichana ili washiriki kikamilifu katika kujenga mustakabali wa taifa.
 
Kuelekea maadhimisho ya siku hiyo, TSN iliandaa shughuli mbalimbali ikiwemo mafunzo ya afya ya akili kwa wafanyakazi wake yaliyohusisha pia wanaume, yenye lengo la kuimarisha ustawi na uwiano mzuri kazini.
 
Pia taasisi hiyo inapanga kutoa msaada kwa watu wenye uhitaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ikiwa ni sehemu ya shughuli zake za kuwafikia jamii wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button