Mradi Kidijitali kuwanufaisha wanawake Lakimoja

ZAIDI ya wanawake 100,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini wanatarajiwa kunufaika na mradi wa miaka mitatu wa uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kupitia teknolojia ya kidijitali, unaolenga kuwawezesha katika masuala ya teknolojia, ubunifu na shughuli za kiuchumi ili kuongeza mchango wao katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Wanawake, Badru Abdunuru, alisema mradi huo utatoa mafunzo ya ujuzi wa kiuchumi na teknolojia kwa wanawake na vijana, sambamba na kuanzisha kituo maalumu cha ubunifu na mafunzo ya teknolojia.
Amesema kituo hicho kitakuwa mahali pa kuwajengea uwezo wanawake na vijana kwa kuwapatia maarifa na stadi za kisasa zitakazowawezesha kushiriki katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma zinazotumia teknolojia. “Lengo letu ni kuhakikisha wanawake, wasichana na vijana ambao wamekuwa wakiachwa nyuma wanapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na matumizi ya teknolojia,” alisema Abdunuru.
Ameongeza kuwa mbali na mafunzo, mradi huo pia utajikita katika kuimarisha mifumo na sera mbalimbali kwa lengo la kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ili kuongeza ushiriki na manufaa kwa wanawake katika nyanja za maendeleo.
“Kupitia ushirikiano huu, Serikali inalenga kuimarisha elimu ya kidijitali, kupanua fursa za ubunifu kwa wanawake, kujenga uwezo wa taasisi na kuendeleza suluhisho za kidijitali zitakazoboresha maisha ya wanawake na makundi yaliyo katika mazingira magumu,” alisema.

Abdunuru amezitaja Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kuwa miongoni mwa taasisi zitakazochangia kufanikisha utekelezaji wa mradi huo.
Amesema taasisi hizo zitasaidia kujenga ujuzi wa kidijitali, kuendeleza ubunifu, kuimarisha ujasiriamali na kuwapa wanawake na wasichana fursa za kushiriki kikamilifu katika sayansi, teknolojia na uchumi wa kidijitali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa GIZ, Anne Hahn, alisema makubaliano hayo yanafungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika kuimarisha usawa wa kijinsia, elimu ya teknolojia na uwezeshaji wa wanawake na vijana nchini.
Amesema mradi huo unatarajiwa kuwafikia wanawake katika maeneo mbalimbali ya nchi huku ukilenga kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi zinazotumia teknolojia na ubunifu. “Tunataka kuona wanawake wengi zaidi wakishiriki katika uchumi wa kidijitali na kutumia fursa za teknolojia za kisasa ili kuboresha maisha yao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema Hahn.

Naye Mkuu wa Uhusiano wa Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Marlene Landes, alisema utekelezaji wa mradi huo unaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia.
“Tunayo furaha kushirikiana na Tanzania katika eneo hili la kuwajengea uwezo wanawake. Tunaamini ushirikishwaji huu utaleta matokeo makubwa kwa wanawake na kuwawezesha kujikita zaidi katika matumizi ya teknolojia,” alisema Landes. SOMA: Wanawake Handeni Mji wafundwa teknolojia kiuchumi
Mradi huo unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika maisha ya wanawake na wasichana nchini kwa kuwawezesha kupata ujuzi wa kidijitali, kuanzisha ubunifu wenye tija na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia. Mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), na utahusisha utoaji wa mafunzo pamoja na matumizi ya teknolojia kwa vitendo.



