Wananchi Simiyu wakumbushwa fursa

MASWA: WANANCHI wa Mkoa wa Simiyu wametakiwa kutumia fursa zinazopatikana kwatika mkoa huo ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwao binafsi na taifa kwa ujumla.
Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi ameeleza hayo leo Machi 7,2026 katika kikao cha Shina namba mbili Kijiji cha Njiapanda Kata ya Isanga wilayani Maswa mkoani Simiyu, ikiwa ni mwanzo wa ziara yake mkoani humo.
Akizungumza katika shino hilo Kihongosi alisema Simiyu ni Mkoa wenye fursa nyingi za maendeleo ambazo zikitumika ipasavyo zinaweza kuwanufaisha wananchi na kuinua uchumi wa eneo hilo.
“Jambo la pili ninalotaka kuwaambia watu wa Simiyu,Mkoa huu una fursa nyingi sana. Tukifanya kazi kwa bidii tutapata mafanikio makubwa sana,” amesema Kihongosi.

Mkoa wa Simiyu unajishughulisha na kilimo hususani cha zao la biashara aina ya pamba kwa kiasi kikubwa, sambamba na shughuli za uchimbaji wa madini na uvuvi kwa kiasi chake.
Kihongosi amesema ili wananchi waweze kuzitumia fursa hizo kikamilifu ni muhimu kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“Bila amani hakuna mtu anaweza kufuga, huwezi kuuza dukani na huwezi kufanya shughuli yoyote ya maendeleo hata miradi ya maji, barabara au umeme,” amesema.
Kihongosi amesisitiza jukumu la kulinda amani si la serikali pekee bali ni la kila mwananchi, akisisitiza chama kitaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha changamoto zinatatuliwa hususani kwenye zao la pamba.

Akisoma ajenda ya shina hilo Katibu wa shina namba mbili, Sitta Makolo amesema ubalozi huo una jumla ya wanachama 50, wakiwemo wanawake 31 na wanaume 19 na ulipaji wao wa ada kw amaaka ni Sh 1200 ambayo ni sawa na Sh 100 kwa mwezi.



