Mitaa yafungwa kabla ya mazungumzo Iran na Marekani

ISLAMABAD, Pakistan — Mitaa ya mji mkuu wa Pakistan, Islamabad, ilikuwa tupu Jumamosi huku vikosi vya usalama vikifunga barabara kabla ya mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Iran na Marekani yanayolenga kumaliza vita vilivyodumu karibu wiki sita.
Mamlaka za Pakistan ziliwataka wakazi kubaki majumbani, hali iliyoufanya mji huo kuonekana kama umewekwa chini ya amri ya kutotoka nje (curfew).
Ujumbe wa Marekani unaongozwa na Makamu wa Rais JD Vance, huku wajumbe wa Iran wakiongozwa na Spika wa Bunge Mohammad Bagher Qalibaf.
Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alisema mzozo huo umeingia katika hatua “ngumu” wakati pande hizo zikijaribu kubadili sitisho la muda la mapigano kuwa makubaliano ya kudumu.
Alionya kuwa mazungumzo hayo yako katika hatua ya “kuamua hatima,” yakimaanisha mafanikio au kushindwa kwake yanaweza kuamua mwelekeo wa mgogoro huo.



