Trump aonya atakayekiuka makubaliano usitishaji vita

UFARANSA: Rais wa Marekani, Donald Trump ametishia kurejea katika mashambulizi na kuwaua maofisa wa Iran iwapo hawatafuata masharti ya makubaliano hayo ya kumaliza vita yaliyosainiwa jana katika mkutano wa G7 nchini Ufaransa.

Makubaliano hayo ya vipengele 14 yanaongeza muda wa kusitishwa kwa mapigano uliotangazwa Aprili kwa siku nyingine 60, ikiwa ni pamoja na Lebanon, ili kuruhusu pande zote mbili kujadili makubaliano ya mwisho ya amani.

Trump na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian wamesaini hati hiyo kwa njia ya kidijitali kwa Kiingereza na Kifarsi, kwa mujibu wa maofisa wa Marekani na Iran, huku wizara ya mambo ya nje ya Iran ikisema makubaliano hayo yameanza kutumika rasmi Jumatano.

Hati hiyo ya makubaliano inajumuisha kusitishwa mara moja kwa vita katika maeneo yote ya mapigano, ikiwemo Lebanon, kurejeshwa kikamilifu kwa usafiri wa majini kupitia mkondo wa Hormuz bila malipo yoyote, kuondolewa kwa mzingiro wa Marekani dhidi ya bandari za Iran, kufutwa kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, kufunguliwa kwa mali za Iran zilizokuwa zimezuiwa, pamoja na kuanzishwa kwa mfuko wa uwekezaji wa dola bilioni 300 kwa ajili ya ujenzi upya wa Iran baada ya vita.

Bei za mafuta ziliendelea kushuka Jumatano kutokana na matarajio ya kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz, njia nyembamba lakini muhimu ya usafiri wa majini kati ya Iran na Oman. Bei ya mafuta ghafi aina ya Brent ilishuka hadi chini ya dola 80 kwa pipa, kiwango cha chini zaidi tangu kuanza kwa vita. Hata hivyo, bei hizo zilirejea kupanda kwa zaidi ya asilimia moja baada ya Trump kutishia kurejea katika vitendo vya kijeshi.

Iran pia imeahidi kutotengeneza silaha za nyuklia, ikisisitiza tena msimamo ambao imekuwa ikiueleza kwa miongo kadhaa. Aidha, imekubali kupunguza kiwango cha urutubishaji wa akiba yake ya urani (enriched uranium) ndani ya nchi chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Hata hivyo, Trump alikuwa ametaka urani hiyo ihamishwe nje ya Iran, jambo ambalo Tehran imekataa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button